IQNA

Waumini 17 wapoteza maisha katika mlipuko wa gesi msikitini Bangladesh

22:39 - September 05, 2020
Habari ID: 3473141
TEHRAN (IQNA)- Waumini wasiopungua 17 wamepoteza maisha katika ajali ya mripuko wa bomba la gesi katika msikiti nchini Bangladesh.

Maafisa wa serikali wamesema leo Jumamosi kuwa, ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia leo katika wilaya ya Narayanganj, nje kidogo ya mji mkuu Dhaka.

Maafisa wa zimamoto wamesema yumkini mripuko huo ulisababishwa na kuvuja kwa bomba la gesi ambalo linapita chini ya msikiti mmoja katika eneo hilo. Waumini 17 wa Kiislamu waliokuwa wakisali katika msikiti huo wameaga dunia katika ajali hiyo, huku wengine 30 wakijeruhiwa.

Samanta Lal Sen, mratibu wa kitengo cha wagonjwa walioungua kwa moto katika hospitali moja ya serikali wilayani Narayanganj amesema miongoni mwa waliopoteza maisha katika ajali hiyo ya jana Ijumaa ni mtoto wa miaka saba.

Amesema yumkini idadi ya wahanga wa mripuko huo wa bomba la gesi ikaongezeka kwa kuwa aghalabu ya majeruhi wapo katika hali mbaya ya kiafya.

Ajali za moto zimekuwa zikishuhudiwa mara kwa mara nchini Bangladesh. Februari mwaka jana, moto uliua watu 78 katika kituo kimoja cha kuwatunza wazee mjini Dhaka, huku wengine 25 wakipoteza maisha katika ajali nyingine ya moto mjini hapo mwezi mmoja baadaye.

3920924

captcha