IQNA

Kikao cha Tehran

Majirani wataka serikali jumuishi iundwe Afghanistan

10:16 - October 28, 2021
Habari ID: 3474482
TEHRAN (IQNA)-Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi JIrani na Afghanistan mwishoni mwa kikao chao hapa Tehran wametoa taarifa ya pamoja na kusisitiza kuwa: njia pekee ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Afghanistan ni kuasisi muundo mpana wa kisiasa kwa kuyashirikisha makundi yote ya nchi hiyo.

Mkutano wa Pili wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi Jirani na Afghanistan pamoja na Russia ulifanyika jana jana Jumatano hapa Tehran na mwishoni mwa mkutano huo kulitolewa taarifa ya pamoja. Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Uzbekistan, Tajikistan, Turkimenistan na Pakistan walihudhuria ana kwa ana katika  mkutano huo hapa Tehran huku Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Russia na China wakihudhuria kwa njia ya intaneti.

Katika taarifa yao ya pamoja, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi Jirani na Afghanistan wamekumbusha misingi iliyoafikiwa kimataifa kuhusu haki za binadamu na kuheshimiwa malengo ya wananchi wa Afghanistan kwa ajili ya kufikia amani ya kudumu  na kusema kuwa: wanataraji kuiona Afghanistan ikiwa nchi yenye  amani, ustawi na maendeleo kwa kuwa na mahusiano na nchi jirani.

Taarifa hiyo ya pamoja katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi Jirani na Afghanistan pamoja na Russia imeitolea wito jamii ya kimataifa na nchi wafadhili kuendelea kuzisaidia kifedha na kutoa misaada ya kutosha na inayotakiwa kwa nchi zinazowapokea wakimbizi wa Kiafghani khususan Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Pakistan na nyinginezo jirani na Afghanistan. 

3476231

captcha