IQNA

Raisi: Hujuma ya hujuma dhidi ya vituo vya mafuta vya Iran ni njama ya maadui

12:04 - October 28, 2021
Habari ID: 3474485
TEHRAN (IQNA)- Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, shambulio la kimtandao (cyber attack) dhidi ya vituo vya mafuta vya Jamhuri ya Kiislamu ni njama za maadui zilizolenga kuwahamakisha na kuvuruga maisha ya kila siku ya Wairani.

Sayyid Raisi alisema hayo jana Jumatano katika kikao cha Baraza la Mawaziri na kuongeza kuwa, hujuma hiyo ya kimtandao ya juzi Jumanne dhidi ya mfumo wa usambajazi mafuta ya petroli ilipania kuwachochea na kuibua ghadhabu miongoni mwa wananchi wa Iran.

Amesisitizia haja ya taifa hili kuwa macho daima na kuwa tayari wakati wote kwa ajili ya kuzima mashambulio kama hayo ya maadui. Amefafanua kwa kusema: Si tu maafisa wa Iran hawakuchanganyikiwa kutokana na shambulio hilo, lakini walilishughulikia tatizo hilo kwa kasi ya juu.

Aidha Rais wa Iran amewapongeza wananchi wa Iran kwa kukabiliana na tatizo hilo, sanjari na kutoruhusu yoyote autumie vibaya mgogoro huo uliojitokeza.

Sayyid Raisi amezitaka mamlaka husika za Iran zisiruhusu kabisa maadui watekeleza njama zao ghalati zenye lengo la kuvuruga maisha ya kila siku ya wananchi wa nchi hii.

Juzi Jumanne, mfumo wa serikali unaosimamia usambazaji wa mafuta ya petroli yaliyowekewa ruzuku ulishambuliwa, lakini kufikia siku hiyo hiyo usiku, tatizo hilo lilikuwa limeshapatiwa ufumbuzi.

Aghalabu ya wananchi wa Iran wanategemea mafuta ya petroli yaliyowekewa ruzuku na serikali ya Jamhuri ya Kiislamu na mafuta hayo hupatikana kwa kutumia kadi maalumu ambayo imeunganishwa na mtandao wa intaneti.

 4008414

captcha