IQNA

Raisi: Iran ina haki isiyopingika ya kutumia teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani

11:11 - April 10, 2022
Habari ID: 3475107
TEHRAN (IQNA)- Sambamba na Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ameshiriki katika maonyesho ya Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran ambapo amezindua mafanikio mapya katika uga wa miradi ya nyuklia yenye malengo ya amani.

Ikumbukwe kuwa Aprili 9 miaka 16 iliyopita, katika mwaka wa 2006 Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilifanikiwa kupata teknolojia ya kurutubisha madini ya urani kwa ajili ya matumizi ya amani katika sekta ya nyuklia. Katika kuenzi jithada zilizojaa fakhari za wanasayansi wa nyuklia wa Iran, siku hii huadhimishwa kila mwaka hapa nchini kama 'Siku ya Kitaifa ya Nishati ya Nyuklia."

Kwa mnasaba wa siku hii, Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameshiriki katika maonyesho ya mafanikio ya nyuiklia ambako amezindua mafanikio tisa mapya ya Iran katika uga wa sayansi ya nyiklia ikiwa ni pamoja na kizazi kipya cha mashinepewa zilizoundwa kikamilifu nchini Iran.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza furaha yake kutokana na mafankio ya vijana wasomi Wairani katika uga wa nyuklia na kusema, mafanikio hayo ni nembo ya kujiamini na kutegemea uwezo wa ndani ya nchi.

Rais wa Iran amesisitiza kuwa, Iran ina haki isiyopingika ya kutumia teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani. Aidha amesema wanasayansi Wairani wamechukua hatua nzuri za utafiti katika sekta ya nyuklia kwa malengo ya amani na hivyo serikali itaendelea kuwaunga mkono. Amesema, katu Iran haiwezi sitisha shughuli zake za nyuklia.

Katika maonyesho hayo ya leo, Shirika la Nishati ya Atomiki Iran limezindua mpango wa kistratijia wa kuzalisha megawati 10,000 za umeme wa nyuklia kwa kutumia vituo vya nishati ya nyuklia vilivyoundwa kikamilifu ndani ya nchi.

4047894

Kishikizo: raisi iran nyuklia
captcha