IQNA

Askari wa utawala wa Kizayuni wavamia Msikiti wa Al Aqsa

11:56 - April 15, 2022
Habari ID: 3475128
TEHRAN (IQNA)- Wanajeshi wa utawala haramu wa Israel mapema leo wameuvamia Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) na kuwajeruhi waumini Wapalestina ikiwa ni katika muendelezo wa uchokozi unaotolezwa na utawala huo dhidi ya Wapalestina katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Taarifa zinasema askari wa Israel waliuvamia Msikiti wa Al Aqsa mapema leo Alfajiri kupitia lango la Al Mughrabi ambapo waliwafyatulia risasi za plastiki waumini waliokuwa msikitini.

Aidha wanajeshi hao wa Israel waliwashambulia wafanyakazi wa ambulensi ambao walifika msikitini hapo kuwasaidia majeruhi. Hilali Nyekundu ya Palestina imeripoti kuwa Wapalestina 90 wamekimbizwa hospitalini kupata matibabu baada ya kujeruhiwa katika hujuma hiyo ya Wazayuni.

Utawala wa Kizayuni wa Israel umezidisha jinai zake dhidi ya Wapalestina katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani na sasa Wapalestina nao wameimarisha harakati zao za mapambano ya kukabiliana na utawala huo dhalimu.

Wakati huo huo, miji ya Ukingo wa Magharibi hasa Jenin tokea mwanzo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani imeshuhudia kushadidi hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel ambapo hadi sasa idadi kubwa ya Wapalestina wameuawa shahidi na wengine kujeruhiwa baada ya kufyatuliwa risasi na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Alhamisi ya jana pia makumi ya vijana Wapalestina katika kitongoji cha Bitaa kusini mwa mji wa Nablus walipambana na askari wa utawala wa Kizayuni ambapo Wapalestina 35 walijeruhiwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya Kipalestina ya Felestin Al Youm, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa utawala wa Israel tokea Aprili mwaka huu wa 2022 katika Ukingo wa Magharibi imefika 17.

4049567

captcha