IQNA

Ugaidi wa Marekani

Iran yailaumu Marekani kwa hujuma ya kigaidi ya Daesh huko Homs, Syria

22:37 - February 19, 2023
Habari ID: 3476586
TEHRAN (IQNA)- Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali jinai ya hivi karibuni ya kundi la kigaidi la ISIS au Daesh katika viunga vya mji wa Homs nchini Syria na kusema: "Utawala wa Marekani unafuatilia sera za undumakuwili katika masuala ya kimataifa ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya ugaidi."

Katika taarifa , Nasser Kan'ani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali jinai ya kuogofya ya kundi la kigaidi la Daesh huko Homs, Syria ambayo imepelekea kuuawa shahidi zaidi ya raia 50 wasio na hatia. Wanajeshi kadhaa wa Syria pia wameuawa shahidi katika hujuma hiyo ya Daesh.

Kan'ani ametuma salamu za rambirambi kwa serikali na taifa rafiki la Syria huku akisisitiza ulazima wa jamii ya kimataifa kuunga mkono kivitendo serikali ya Syria katika mapambano dhidi ya mabaki ya magaidi wa Daesh.

Hali kadhalika amesema Marekani kama serikali ambayo iliibua na kuliunga mkono kundi la kigaidi la Daesh na pia kama serikali ambayo ina wanajeshi kinyume cha sheria katika baadhi ya maeneo ya Syria ni mshirika wa muendelezo wa jinai za Daesh nchini humo.

Taarifa zinasema kuwa magaidi wa Daesh waliwaua raia hao waliokuwa wanakusanya uyoga mwitu katika milima ya mkoa huo.

Vyombo vya habari vya Syria vinasema hadi sasa waliopoteza maisha katika jinai hiyo ya Daesh wamefikia 53.

4122978

captcha