IQNA

Jinai za Israel

Iran yasisitiza kuhusu mkutano wa dharura wa nchi za Kiislamu ili kutetea Palestina

18:43 - April 08, 2023
Habari ID: 3476835
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amefanya mazungumzo ya simu na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na kutoa wito wa kuitishwa kikao cha dharura cha jumuiya hiyo ili kukabiliana na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa.

Mapema Jumatano, tarehe 5 Aprili, wanajeshi wa Kizayuni waliwashambulia Waislamu waliokuwa katika ibada ya Itikafu ndani ya Msikiti wa Al-Aqsa na kuwalazimisha Waislamu hao kutoka nje ya eneo hilo la ibada. Katika shambulio hilo idadi kadhaa ya Wapalestina walijeruhiwa.

Katika mazungumzo ya Hossein Amir-Abdollahian na Katibu Mkuu wa OIC, Hussein Ibrahim Taha, maafisa hao wamejadili na kubadilishana mawazo kuhusu mashambulizi ya Israel dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa na kuvunjiwa heshima eneo hilo tukufu ambalo ni kibla cha kwanza cha Waislamu.

Katika mazungumzo hayo ya simu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza ulazima wa kufanyika kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu katika ngazi ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama ili kujadili njia za kukabiliana na shambulio la hivi karibuni la utawala wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa. Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kwa ushirikiano wowote katika kuitisha mkutano huu.

Amir Abdollahian ameashiria pia mazungumzo ya simu ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Ebrahim Raisi, na Rais wa Indonesia, Joko Widodo, kuhusiana na suala hilo na kumfahamisha Katibu Mkuu wa OIC kuhusu mipango mingine ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na suala hilo.

Kwa upande wake, Hussein Ibrahim Taha amelaani shambulio la hivi karibuni la Wazayuni dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa na kusema kuwa kikao cha wawakilishi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo kitafanyika kesho Jumapili katika ngazi ya Kamati ya Utendaji kwa ajili ya kushughulikia suala hilo. 

Jumatano iliyopita, askari wa utawala haramu wa Israel walivamia Msikiti wa al Aqsa kwa mara ya pili mfululizo na kujaribu kuwafukuza waumini wa Kipalestina katika msikiti huo kwa kurusha maguruneti na kumimina risasi.

Video za uvamizi huo zinaonyesha wanajeshi wa Israel wakiwapiga kikatili waumini wasio na ulinzi kwa kutumia marungu na bunduki. Makumi ya Wapalestina walijeruhiwa na wengine kukamatwa katika shambulio hilo.

4131988

Kishikizo: iran palestina oic
captcha