IQNA

Jinai za Israel

Wapalestina hawana imani na sheria za kimataifa kwani hazizuii Israel kuua watoto

17:56 - November 21, 2023
Habari ID: 3477926
TEHRAN (IQNA) - Mwanaharakati wa Gaza na mkuu wa shirika la kutoa misaada anasema Wapalestina hawawezi tena kuamini sheria za kimataifa kwani zimeshindwa kuwalinda watoto ambao wanakabiliwa na uvamizi wa kikatili wa Israel.

"Leo, hatuwezi kuamini maneno kuhusu sheria za kimataifa na haki za binadamu. Hatuwezi kuamini sheria kuhusu haja ya kuheshimu haki za wanawake na raia na kuwalinda wakati wa migogoro ya silaha. Hatuwezi kuamini Mikataba ya Geneva na ahadi zake,” Saleh Al-Kashif, Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Charitable Association For Palestinian Relief, aliiambia Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) siku ya Jumatatu.

Vita vya maangamizi ya umati vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza uliozingirwa tangu tarehe 7 Oktoba umeua watu wasiopungua 13,300, wakiwemo watoto zaidi ya 5,000, huku jumuiya ya kimataifa ikishindwa kukomesha ukatili wa utawala huo ghasibu.

"Ikiwa ulimwengu unataka makubaliano haya, mikataba, na madai ya kimataifa kubaki halali na ya kuaminika kwa watu wa Palestina na Waislamu, lazima wachukue hatua haraka na kuokoa watoto, wanawake na raia huko Gaza," alisisitiza.

Al-Kashif alisema jumuiya ya kimataifa "lazima ichukue hatua za kivitendo na kuwapatia Wapalestina msaada wa kimataifa. Pia wanapaswa kuwawajibisha watawala wahalifu wa Israel walioua watu hao wasio na hatia na kuwafungulia mashitaka kwa makosa yao.”

Matamshi hayo yametolewa wakati watu duniani kote wakiadhimisha tarehe 20 Novemba kama siku ya watoto duniani.

“Leo ni tarehe 20 Novemba, Siku ya Watoto Duniani, lakini tunaona janga la kutisha kwa watoto wa Kipalestina. Wanauawa na kunyimwa haki za msingi za maisha. Wanapoteza wazazi na nyumba zao na wanakabiliwa na mashambulizi ya kikatili. Hawajafanya chochote kibaya isipokuwa kuishi na kupumua katika ardhi yao wenyewe, Palestina, na kusisitiza kuendelea na maisha yao huko," mwanaharakati huyo alisema.

Mwanaharakati huyo amekosoa kutochukua hatua vyombo vya kimataifa katika kuwalinda watoto wa Kipalestina. “Je, ni kwa jinsi gani Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNICEF, na mashirika mengine ya kitaifa yanadai kuwajali watoto na haki zao, wakati hatuoni hatua zozote za kweli kwa haki za watoto hawa huko Gaza? Inaonekana kwamba tarehe 20 Novemba ni ya watoto wa Magharibi pekee, si ya watoto wa Gaza, Palestina, na ulimwengu wa Kiislamu.”

Pia ameashiria haja ya kuongeza ufahamu kuhusu watoto wa Kipalestina kote duniani. "Sote tuna jukumu la kuwatetea watoto hawa na kujulisha ulimwengu kuhusu hali zao."

“Tunapaswa pia kudai hatua za kisheria kutoka kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNICEF, na mashirika mengine duniani kote. Tunapaswa kufichua jinai za utawala wa Israel na kutangaza kuwa watoto wa Gaza wako katika hatari ya mauaji ya halaiki na mauaji ya umati,” akasisitiza.

Al-Kashif pia alipongeza maandamano ambayo yamefanyika katika mitaa ya nchi za Magharibi kuunga mkono Palestina katika wiki chache zilizopita, hata hivyo, alibainisha kuwa "bado hayajaweza kuweka shinikizo la kweli kwa serikali za Magharibi."

"Serikali hizi zinaendelea kuunga mkono na kuisaidia Israel na kuipatia silaha," alilalamika, akitaka kuongezwa mashinikizo zaidi kwa waungaji wa utawala katili wa Israel.

captcha