IQNA

Mwezi wa Ramadhani

Mamia ya wanawake wapata mafunzo ya kutoa msaada katika Msikiti wa Mtume

19:20 - March 09, 2024
Habari ID: 3478473
IQNA - Msururu wa kozi za mafunzo zimefanyika hivi karibuni ili kuwafundisha wanawake 1,352 wanaojitolea kuwasaidia waumini wanaoelekea kwenye Msikiti wa Mtume yaani Al-Masjid an-Nabawi, eneo la pili kwa utakatifu katika Uislamu, katika mji wa Madina, Saudi Arabia.

Kozi hizo za mtandaoni, zilizoandaliwa na Mamlaka Kuu ya Kusimamia Al-Masjid an-Nabawi, zililenga kufundisha wafunzwa ujuzi wa mawasiliano na namna ya kuwaongoza waumini wanawake.

Mada zilizoshughulikiwa katika kozi hizo zilijumuisha ujuzi wa kazi ya kujitolea, usimamizi wa umati, kuwasaidia waumini wanaohitaji na kuwatunza wazee na watu wenye matatizo ya kimwili.

Kozi hizo ziliandaliwa kabla ya Ramadhani, waliohitimia wanatazamiwa  kuanza kazi zao Jumatatu.

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kawaida huashiria msimu wa kilele wa Umrah au hija ndogo Msikiti Mkuu wa Makka, Al Masjid Haram., eneo takatifu zaidi ya Uislamu, katika jiji la Makka.

Baada ya kufanya Umra, mahujaji wengi huelekea Madina kuswali katika Msikiti wa Mtume Muhammad SAW na kuzuru maeneo mengine ya Kiislamu mjini humo.

Viongozi wa Saudia wanaosimamia Al-Masjid an-Nabawi wamesema wamejiandaa kwa ajili ya kuwahudumia waumini wanaotarajiwa kumiminika kwa wingi mahali hapo mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Zaidi ya milo milioni 8.5 ya Iftar inakadiriwa kusambazwa miongoni mwa waumini baada ya kumalizika katika kipindi chote cha mwezi wa Ramadhani katika msikiti huo mtakatifu wa Madin.a

Kiasi cha chupa milioni 2.5 za maji yaliyobarikiwa ya Zamzam zitatolewa msikitini wakati wa  Ramadhani.

Katika kuelekea Ramadhani, Mamlaka Kuu ya Kusimamia Al-Masjid an-Nabawi hivi karibuni ilifanya warsha ambayo maandalizi ya mwezi huo yalikaguliwa. Ni pamoja na kuimarisha huduma ili kukabiliana na ongezeko linalotarajiwa la idadi ya waumini.

Zaidi ya Waislamu milioni 280 walisali katika Msikiti wa Mtume mnamo 2023, kulingana na takwimu rasmi.

Msikitini hapo pia kuna eneo la Al Rawda Al Sharifa, ambapo kuna kaburi la Mtume Muhammad (SAW).

3487477

Habari zinazohusiana
captcha