IQNA

Ahadi ya Kweli

Msomi wa Yemen: 'Ahadi ya Kweli' haikuwa tu operesheni ya kulipiza kisasi

22:59 - April 17, 2024
Habari ID: 3478695
IQNA - Profesa wa chuo kikuu cha Yemeni amesema "Operesheni ya Ahadi ya Kweli" ya kijeshi ya Iran dhidi ya Israeli ilikuwa zaidi ya shambulio la kulipiza kisasi.

Akizungumza na IQNA, Sayyid Ibrahim al-Shami amesema operesheni hiyo ni hatua ya kishujaa na tukufu iliyochukuliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo taathira zake zinahisika kieneo na duniani kote.

Amesema ni tukio kubwa la kihistoria katika kipindi cha mapambano baina ya Wapalestina wanaopigania ukombozi na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unakalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Al-Shami amebainisha kuwa, shambulio hilo halijawahi kutokea katika historia ya utawala ghushi wa Israel, utawala ambao umekua na tabia ya dhulma, majivuno na kutojua mistari myekundu na umekuwa ukiungwa mkono kijeshi na kisiasa na madola ya kibeberu hususan Marekani. .

Amesema iwapo mtu anataka kuashiria mafanikio makubwa zaidi ya operesheni hiyo ya Iran, itakuwa ni kuvunjika kwa taswira ya nguvu ya kutoshindwa ambayo utawala wa Kizayuni ulitaka kuidhihirisha.

Operesheni hiyo ilikuwa mwanzo wa awamu mpya ya kuporomoka kwa utawala wa Kizayuni, mwanazuoni huyo ambaye pia ni kiongozi wa sala katika kitongoji cha Sana’a aliendelea kusema.

Leo, ameongeza kuwa, mhimili wa upinzani kuanzia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hadi Yemen, Iraq, Lebanon na Syria unaonekana kuwa na nguvu zaidi kuliko hapo awali.

Katika kujibu shambulio la utawala wa Kizayuni dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran huko Damascus, mji mkuu wa Syria, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alfajiri ya Jumapili ya tarehe 14 April 2024 imefanya mashambulizi ya moja kwa moja ya ndege zisizo na rubani na makombora katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) lilitekeleza mashambulizi hayo makubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi Israel, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutumia silaha hizo dhidi ya malengo halisi.

Operesheni ya mashambulizi hayo ya kulipiza kisasi, yaliyopewa jina la Ahadi ya Kweli ilisababisha uharibifu mkubwa katika kambi za kijeshi za Israel.

Jioni ya tarehe 1 Aprili 2024, utawala wa Kizayuni ulishambulia ubalozi mdogo wa Iran huko Damascus na kupelekea kuuawa shahidi washauri saba wakuu wa kijeshi wa Iran. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu alikitaja kitendo hicho cha Tel Aviv kuwa ni shambulio dhidi ya ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni utaadhibiwa. 

Kilichofanywa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni hatua ya "kuiadhibu" Israel na ni katika hatua ya "kujitetea halali" kwa mujibu wa  kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa.

 4210641

Habari zinazohusiana
Kishikizo: Ahadi ya Kweli irgc
captcha