IQNA

Al Azhar yapongezwa kwa kuasisi kituo cha kukurubisha madhehebu ya Kiislamu Misri

10:50 - May 14, 2016
Habari ID: 3470311
Wanazuoni wa Kishia nchini Misri wamepongeza Chuo Kikuu cha Al Azhar kwa hatua yake ya kuasisi kituo cha kukurubuisha madhehebu ya Kiislamu.

Ahmed Rasim al-Nafis, msomi na kiongozi mwandamizi wa Mashia nchini Misri ameunga mkono hatua ya Al Azhar kubuni Kituo cha Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu na kusema hatua hiyo ni mpango mpya ambao unaleta matumaini ya kuimarisha umoja baina ya madhehebu za Kiislamu na kukabiliana na wanaozusha fitina.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, ameongeza kuwa, kuwaita Waislamu wote wawe kitu kimoja ni hatua nzuri na inayokubalika. Amesema anaunga mkono mpango huo na akitakiwa ktoa ushirikiano wake atafanya hivyo.

Siku ya Alkhamisi Sheikh Ahmed Karima, mhadhiri wa fikihi na sheria ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha al Azhar alisema kuwa, iwapo madhehebu mbalimbali ya Kiislamu yatakurubiana na kudumisha umoja baina yao, itakuwa rahisi kutekelezwa sheria tukufu za Uislamu na kupatikana umoja kati ya Waislamu wote.

Amesema karibuni hivi kutaanzishwa taasisi maalumu ya kuyakurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu nchini humo. Amesema, maulamaa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha al Azhar ndio watakaoasisi taasisi hiyo. Hata hivyo amekataa kutangaza majina ya maulamaa na wanafunzi wa kidini watakaounda taasisi hiyo.

Sheikh Ahmed Karima, ni miongoni mwa maulamaa walio mstari wa mbele katika kupigania umoja na mshikamano baina ya Waislamu. Aliwahi kunukuliwa akiwashukuru Waislamu wa Kishia nchini Iran kwa kuishi kwa salama na amani na ndugu zao wa Kisuni na kumshukuru pia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei kwa uungwana wake mkubwa katika suala hilo.

Sheikh Ahmed Karima amenukuliwa akisema ameshuhudia kwa macho yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akigharamia kifedha madrasa na shule za kidini za Kisuni katika mkoa wa Kurdistan kwa ajili ya kueneza mafundisho ya Waislamu wa madhehebu ya Kisuni nchini Iran. Alimshukuru pia Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa fatwa yake maarufu ya kuharamisha kuvunjiwa heshima maswahaba na wake wa Bwana Mtume Muhammad SAW.

3497670

captcha