IQNA

Waislamu wa Myanmar wakatiwa misaada ya chakula

18:51 - October 20, 2016
Habari ID: 3470623
Serikali ya Myanmar imezuia misaada ya chakula kufikishwa kwa Waislamu wa kabila la Rohingya wanaoishi katika jimbo la Rakhine kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Kwa mujibu wa mashuhuda, vikosi vya jeshi la Myanmar vimewekwa katika maeneo ya kaskazini mwa jimbo la Rakhine na karibu na mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Bangladesh na kwamba hawaruhusu kufikishwa misaada ya chakula katika eneo hilo ambalo wakaazi wake waliowengi ni Waislamu.

Kufuatia mauaji yaliyotokea mwanzoni mwa wiki iliyopita ya askari polisi tisa wa Myanmar waliouawa karibu na mpaka wa Bangladesh, serikali ya Myanmar imechukua hatua kali zaidi za usalama katika jimbo la Rakhine na kudai kwamba Waislamu wa kabila la Rihingya ndio waliohusika na mauaji hayo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani limetangaza kuwa kila siku limekuwa likitoa misaada ya chakula kwa watu kati ya elfu 80 hadi 85 katika maeneo yaliyozingirwa na jeshi, lakini katika siku za karibuni jeshi hilo limezuia kufikishwa misaada hiyo ya chakula katika maeneo hayo.

Arsin Sahakiyan, mwakilishi wa WFP nchini Myanmar amesema wanajeshi wametawanywa kila mahala na marufuku ya kutotoka nje inatekelezwa hivyo ni jambo lisilowezekana kuyafikia maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache duniani inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi. Serikali ya Myanmar inakataa kuwapa haki za uraia Waislamu ambao idadi yaoni zaidi ya watu milioni moja na laki tatu.

Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Thailand, Malaysia na Indonesiakutokana na mashambulio ya Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.

Hivi karibuni afisa wa ngazi za juu katika Umoja wa Mataifa amesema Waislamu Zaidi ya 120,000 nchini Myanmar wanaishi katika hali mbaya sana wakiwa katika kambi za wakimbizi wa ndani ya nchi. Stephen O'Brien, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kibinadamu alisema kufuatia machafuko ya hivi karibuni katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar, Waislamu wanakabiliwa na hali mbaya na kunapaswa kuchukuliwa hatua za haraka kuwalinda na kuzuia machafuko Zaidi eneo hilo. Aliseam alishuhudia kwa macho yake hali mbaya ya Waislamu ambao wanaishi kwa umasikini mkubwa huku wakiteswa na wakinymwa haki zao na utawala wa Myanmar.

/3539366
Kishikizo: waislamu myanmar iqna
captcha