IQNA

Waziri wa masuala ya kidini Tunisia afutwa kazi kwa kukosoa Uwahhabi

8:06 - November 05, 2016
Habari ID: 3470652
Waziri wa Masuala ya Dini Tunisia amefutwa kazi, baada ya kusema kuwa, idiolojia ya Uwahhabi ambayo inatawala Saudi Arabia ndiyo chanzo cha ugaidi duniani.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Yousuf Shahid, Waziri Mkuu wa Tunisia amemfuta kazi Abdul Jalil Bin Salim, kwa kile kinachodaiwa kuwa 'ameshambulia misingi ya udiplomasia'.

Akihutubu Jumatano Kamisheni ya Haki, Uhuru na Uhusiano wa Kigeni ya Bunge la Tunisia, Abdul Jalil Salim alitamka bayana kuwa, mfumo wa Saudi Arabia unazalisha ugaidi na misimamo mikali.

Waziri wa Masuala ya Dini wa Tunisia aliwataka viongozi wa Saudi Arabia kurekebisha siasa zao ambazo amesisitiza kuwa lengo lake kuu ni kutengeneza watu wenye misimamo mikali na magaidi.

Waziri huyo aliyepigwa kalamu alifafanua kuwa, fikra za kuwakufurisha Waislamu wengine hazipatikanikatika madhehebu yoyote ya Kiislamu isipokuwa madhehebu ya Kihanbali na kundi la Kiwahabi na kwamba historia inathibitisha kuwa ugaidi nizao lililotokana na fikra za kidini za Suadia.

Kadhalika Abdul Jalil Bin Salim amewahi kunukuliwa na idhaa moja ya kibinafsi ya Mosaique FM akiitaka Saudia kufanya mageuzi katika vyuo vyake akisisitiza kuwa ugaidi kihistoria umezaliwa vyuoni hapo.

Saudi Arabia inatuhumiwa na wengi kuwa muungaji mkono mkuu wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh. Kundi hilo linalowakufurisha Waislamu wote wasioafikia misimamo yake hutegemea misingi ya Uwahhabi katika kuendesha shughuli zake za ugaidi.

Magaidi wanaopata himaya na misaada ya kigeni walianzisha vita dhidi ya Syria mwaka 2011. Serikali ya Syria inasema baadhi ya nchi za Magharibi na waitifaki wao katika eneo la Mashariki ya Kati hasa Uturuki, Saudi Arabia, Qatar na Utawala haramu wa Israel ndio waungaji mkono wakuu wa makundi ya kigaidi kama vile ISIS au Daesh na Jabhatu Nusra.

Serikali ya Tunisia imemfuta kazi waziri huyo wakati yenyewe imekiri kuwa raia wake wapatao 3000 wamejiunga na kundi la ISIS nchini Syria na Iraq na maeneo mengineyo duniani na kwamba wakirejea nyumbani watakuwa ni hatari kwa usalama wa nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika.

3543293

captcha