IQNA

Utawala wa Nigeria wabomoa kituo kingine cha harakati ya Kiislamu

6:23 - November 20, 2016
Habari ID: 3470686
IQNA-Utawala wa kiimla Nigeria umeendeleza ukandamizaji dhidi ya Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo kwa kubomoa vituo kadhaa kadhaa ya harakati hiyo.

Viongozi wa harakati ya Kiislamu ya Nigeria wamesema vyombo vya dola vimebomoa majengo kadhaa ya harakati hiyo ikiwemo skuli, hospitali na vituo vya masomo ya dini katika miji ya Zaria na Saminaka katika jimbo la Kaduna kaskazini mwa nchi hiyo.

Viongozi hao wa harakati ya Kiislamu Nigeria aidha wamebainisha kuwa ubomoaji huo umefanyika bila ya kutolewa taarifa kabla na ilhali harakati hiyo haikuwa imefanya kitendo chochote cha kuichochea serikali kuchukua hatua ya kijinai ya kusababisha maafa kama hayo.

Ubomoaji huo umefanywa baada ya vikosi vya usalama vya Nigeria kuwaua wanachama wapatao 100 wa harakati ya Kiislamu waliokuwa wakishiriki kwenye maombolezo ya Arubaini ya Imam Hussein (AS).

Katika tukio hilo lililotokea siku ya Jumatatu, askari usalama wa Nigeria waliwashambulia Waislamu wa Kishia waliokuwa katika maombolezo hayo kwa kutumia risasi moto na mabomu ya kutoa machozi. 

Tangu mwaka uliopita hadi sasa harakati ya Kiislamu Nigeria na wafuasi wake wamekuwa wakikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa serikali ya nchi hiyo.

Miezi 11 iliyopita, yaani Desemba mwaka jana, Jeshi la Nigeria liliwashambulia wafuasi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria katika mji wa Zaria jimboni Kaduna kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Jeshi hilo lilidai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inayoongozwa na Allamah Sheikh Ibrahim Zakzaky walikuwa na njama ya kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi la Nigeria, madai ambayo yamekanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo. Jeshi hilo katili liliizika miili ya waliouawa katika kaburi moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo. Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo huku Sheikh Zakzaky, ambaye hali yake ni mahututi, akiendelea kushikiliwa korokoroni pasina kufunguliwa mashtaka.

3546908


captcha