IQNA

Katika msafara ya Arubaini ya Imam Hussein AS

Waislamu zaidi ya 100 wauawa na Jeshi la Nigeria mjini Kano

22:37 - November 14, 2016
Habari ID: 3470676
IQNA- Jeshi la Nigeria limeua Waislamu zaidi ya100 wa madhehebu ya Shia kwa kuwapiga risasi kiholela kaskazini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Waislamu hao wameuawa walipokuwa katika matembezi ya maadhimisho ya Arubaini ya Imam Hussein AS, nje kidogo ya mji wa Kano ulioko kaskazini mwa Nigeria. Waislamu wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Kamishna wa polisi katika mji huo, Rabiu Yusuf amedai kuwa, mauaji hayo yametokea baada ya Waislamu hao kuwashambulia polisi kwa kutumia silaha baridi kama mapanga na mishale. Hata hivyo watu walioshuhudia wanakadhibisha madai hayo na kusema, polisi waliwashambulia Waislamu hao waliokuwa katika maandamano ya amani.

Aidha katika taarifa, msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Ibrahim Musa amethibitisha kuwa Jeshi la Nigeria liliwafyatulia risasi kiholela.

Maadhimisho ya siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein AS na masahaba zake ambao walitoa mhanga roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika jangwa la Karbala.

Mauaji hayo ya leo mjini Kano yanafanyika wakati ambao miezi 11 iliyopita, yaani Desemba mwaka jana, Jeshi la Nigeria liliwashambulia wafuasi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria katika mji wa Zaria jimboni Kaduna kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Jeshi hilo lilidai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inayoongozwa na Allamah Sheikh Ibrahim Zakzaky walikuwa na njama ya kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi la Nigeria, madai ambayo yamekanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo. Jeshi hilo katili liliizika miili ya waliouawa katika kaburi moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo. Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo huku Sheikh Zakzaky, ambaye hali yake ni mahututi, akiendelea kushikiliwa korokoroni pasina kufunguliwa mashtaka.

3461501

captcha