IQNA

Hofu kuhusu hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky

23:27 - September 09, 2016
Habari ID: 3470554
Waislamu nchini Nigeria wameendelea kufanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi hiyo na kuelezea wasiwasi walionao kuhusiana na hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Waandamanaji hao wameendelea kusisitiza juu ya takwa lao la kuachiliwa huru mwanazuoni huyo wa Kiislamu ambaye kwa miezi kadhaa sasa anashikiliwa na vikosi vya usalama bila ya kufunguliwa mashtak,a huku kukiweko na taarifa kwamba, hali yake ya kiafya ni mbaya.

Wakati huo huo, maandamano ya Waislamu nchini Nigeria ya kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky yameendelea kukandamizwa na vikosi vya usalama vya nchi hiyo ambavyo vinatuhumiwa kwa kukiuka haki za raia.

Aidha maandamano hayo yanaendelea kushuhudiwa nchini humo katika hali ambayo, hivi karibuni Mahakama Kuu ya Nigeria ilikataa ombi lililotolewa na mawakili la kutaka kuachiliwa huru mara moja Sheikh Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, mashirika ya kutetea haki za binadamu ya kimataifa yamekuwa yakitahadharisha mara kwa mara kuhusiana na kuzorota hali ya afya ya kiongozi huyo wa Kiislamu.

Mamia ya wafuasi wa Sheikh Zakzaky, wakiwemo wanawe watatu, waliuawa katika mashambulizi makubwa yaliyofaywa na jeshi la Nigeria dhidi ya makazi ya Sheikh Zakzaky na vilevile kituo chake cha kidini katika mji wa Zaria jimboni Kaduna mnamo tarehe 14 Disemba 2015.

Kiongozi huyo na wanachama wengine kadhaa wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wangali wanashikiliwa na vyombo vya usalama vya nchi hiyo. 

Waislamu nchini Nigeria wameendelea kuilaumu serikali ya Rais Muhammadu Buhari na vyombo vya usalama vya nchi hiyo kwamba, vinawakandamiza Waislamu.

3528387


captcha