IQNA

Mahakama ya Juu Nigeria yakataa kumuachilia huru Sheikh Zakzaky

7:28 - September 01, 2016
Habari ID: 3470542
Mahakama ya Juu Nigeria imepinga ombi lililotolewa la mawakili wa nchi hiyo la kutaka kuachiliwa huru mara moja Sheikh Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
Mahakama hiyo imepinga kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky katika hali ambayo Waislamu wa Nigeria wamekuwa wakifanya maandamano makubwa ya kushinikiza kuachiliwa huru mwanazuoni huyo wa Nigeria, katika miji kadhaa ya nchi hiyo ikiwemo ya jimbo la Kaduna, lililo kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Waandamanaji ambao wamekuwa wakishiriki maandamano hayo wamekuwa wakipiga nara za kutaka kuachiliwa mara moja Sheikh Zakzaky pamoja na wanazuoni wengine wa Kiislamu waliokamatwa pamoja naye na vilevile kutaka jeshi liwakabidhi miili ya watu waliouawa ili wapate kuizika kwa mujibu wa sheria za Kiislamu. Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inasema kuwa ni jambo lisilokubalika kwa nchi inayodai kuzingatia demokrasia na serikali kula kiapo cha kulinda maisha ya wanachi, watu 347 kuuawa kinyama na jeshi na kisha waliohusika na jinai hiyo kutowajibishwa kisheria. Maandamano ya Waislamu wa Kishia wa Nigeria yanaendelea katika hali ambayo hata mashirika ya kutetea haki za binadamu ya kimataifa yamekuwa yakitahadharisha mara kwa mara kuhusiana na kuzorota hali ya afya ya kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu.

Siku chache zilizopita mashirika hayo yalionya kwamba Sheikh Ibrahim Ya'qub Zakzaky anaendelea kushikiliwa katika mojawapo ya jela za Nigeria bila ya kupewa matibabu yanayofaa katika hali ambayo hali yake ya kiafya inazidi kuzorota. Mashirika hayo ya kimataifa yanatahadharisha kwamba iwapo hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky itaendelea kupuuzwa na kutopewa madaktari wa kumshughulikia ni wazi kuwa maisha yake yatakuwa hatarini. Kufikia sasa Waislamu wengi wa Nigeria wamebainisha wazi wasiwasi wao kuhusiana na mwanazuoni huyo wa Kiislamu kuendelea kushikiliwa kwenye jela za nchi hiyo bila kufunguliwa mashtaka.

Waislamu hao vilevile wanataka mwanazuoni huyo aruhusiwe kutembelewa na familia yake na kupewa matibabu yanayofaa haraka iwezekanavyo. Vyanzo vya kuaminika vinasema kwamba jicho la Sheikh Zakzaky liko kweye hali mbaya na halioni kabisa kutokana na jeraha alilopata baada ya kufyatuliwa risasi na jeshi wakati wa kukishambuli kituo chake cha kidini na kwamba serikali haiko tayari kuruhusu madaktari walitibu. Kwa kuzingatia hali hiyo wataalamu wa mambo wanasema kuwa lengo la serikali kuendelea kumshikilia mwanazuoni huyo mashuhuri ni kudhoofisha na hatimaye kuvunjilia mbali Harakati ya Kiislamu ya Nigeria katika miji tofauti ya nchi hiyo.

Awali Sheikh Ismail Shuab, Naibu wa Sheikh Zakzaky alikuwa amesema kwamba katika hali ya hivi sasa kanali kadhaa za Mawahhabi zinashirikiana na serikali ya Nigeria dhidi ya kiongozi huyo wa Harakati ya Kislamu. Mamia ya wafuasi wa Sheikh Zakzaky, wakiwemo wanawe watatu, waliuawa kinyama kufuatia hujuma iliyofaywa na jeshi la Nigeria dhidi ya makazi ya Sheikh Zakzaky na vilevile kituo chake cha kidini katika mji wa Zaria jimboni Kaduna mnamo tarehe 14 Disemba 2015.

Katika hujuma hiyo ambayo mkewe Zakzaky pia alikamatwa, jeshi lilitumia ukatili wa kupindukia ambapo liliua kwa risasi zaidi ya watu 1000 na pia kuteketeza maelfu ya wengine au kuwafanya watoweke.

Hivi karibuni mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu likiwemo la Human Rights Watch yalitaka serikali ya Abuja itekeleze mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Uchunguzi ya Nigeria na kuwahukumu wahalifu wote jeshini waliohusika na mauaji ya mamia ya Waislamu katika mji wa Zaria. Kamati hiyo ililituhumu jeshi kwa kuwaua Waislamu 347 wa Nigeria na kisha kuwazika kwenye makaburi ya umati katika mji wa Kaduna mwishoni mwa mwaka uliopita.

3526879


captcha