IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Rais wa Marekani acheza densi na kinara wa ukoo kisha akosoa uchaguzi wa watu milioni 40 Iran

23:16 - June 05, 2017
Habari ID: 3471009
TEHRAN (IQNA)-Rais wa Marekani acheza densi na kinara wa ukoo kisha akosoa uchaguzi wa Wairani milioni 40

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema rais wa Marekani amecheza densi ya upanga na kinara wa ukoo kisha wakati huo huo anakosoa uchaguzi huru uliowashirikisha Wairani milioni 40.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo Jumapili mjini Tehran alipohutubu katika hauli ya mwaka wa 28 tangu alipoaga dunia mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini (MA) ambayo imefanyika kwenye haram takatifu ya kiongozi huyo.

Ayatullah Khamenei aidha amesema msingi wa kifikra wa harakati ya Imam Khomeini MA ulijengeka katika kuhitimisha satwa ya Marekani nchini Iran. Amesema vijana wa nchi ambazo serikali zao ziko chini ya satwa ya Marekani nao pia wanaichukua Marekani. Amesema kuna gharama ndogo katika kukabiliana na Marekani huku kukiwa na gharama kubwa kwa nchi ambazo zinajipendekeza na kujikurubisha kwa Marekani. Ametoa mfano wa Saudi Arabia ambayo imelazimika kutoa rushwa ya mabilioni ya dola ili kujikurubisha kwa rais mpya wa Marekani.

Akibainisha zaidi Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa: "Tizama namna adui wetu alivyo mchafu. Rais wa Marekani anasimama na kinara wa ukoo na kucheza densi ya upanga katika mfumo wa kikabila wenye uozo na ulio nyuma. Lakini, wanakosoa kura ya Wairani milioni 40 walioshiriki katika uchaguzi huru.”

Ayatullah Khamenei ameendelea kwa kuashiria uungaji mkono wa Marekani kwa hujuma ya Saudia Yemen na kusema: "Mbele yetu tuna maadui ambao wamefika kiwango hiki cha uovu na utovu wa maadili; wanasimama mbele ya wauaji wa raia wa Yemen na wakati huo huo wanazungumza kuhusu haki za binadamu. Je kuna uchafu mbaya zaidi ya huu? Kampeni ya kudondosha mabomu Yemen imekuwa ikiendelea kwa muda wa miaka miwili na nusu sasa. Hawalengi maeneo ya kijeshi bali wanadondosha mabomu katika masoko, misikiti na nyumba za raia. Watu wasio na hatua wamepoteza maisha. Kisha tunasikia wavamizi wakitoa hotuba kuhusu haki za binadamu na kuiwekea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikwazo kwa madai ya ‘haki za binadamu.’”

Kiongozi Muadhamu amebaini kuwa: "Leo, kwa masikitiko, ndugu zetu Yemen, Bahrain, Syria na Libya wanakabiliwa na matatizo wakati wa mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani. Kwa miaka miwili na nusu Saudia imekuwa ikidondosha mabomu Yemen. Lakini wafahamu kuwa hata wakiwadondoshea mabomu watu wa Yemen kwa muda wa miaka 20 hawawezi kufaulu. Tunaamini maadui ndio walioleta vita Syria, Bahrain, Yemen na maeneo mengine ya ulimwengu wa Kiislamu.” Kiongozi Muadhamu amesema suluhisho ni mazungumzo na kusitisha usafirishaji silaha katika nchi hizo.

Ayatollah Khamenei pia amekosoa uingiliaji kijeshi wa Saudi Arabia nchini Bahrain na kusema: "Watu wa Bahrain wanaweza kusuluhisha matatizo yao. Hatua ya Saudia kutuma majeshi yake Saudia ni kinyume cha mantiki. Utawala wa Saudia kamwe hautafanikiwa kwa njia hiyo, hata ukiipa Marekani rushwa ya mabilioni ya dola.”

Kwingineko katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu alitahadharisha kuhusu njama zenye lengo la kupotosha shakhsia ya Imam Khomeini (MA) na mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa, Imam Khomeini alifikia malengo ya harakati zake adhimu ambayo alikuwa akiyalingania kabla ya kufikiwa ushindi wa mapinduzi hayo.

3606322

captcha