IQNA

Waislamu nchini Myanmar wanyimwa haki ya upigaji kura

21:58 - February 13, 2015
Habari ID: 2846218
Serikali ya Myanmar imetangaza kuwa, Waislamu wa kabila la Rohingya hawana haki ya kupiga kura katika kura ya maoni ya katiba ya nchi hiyo.

Rais Thein Sein ametangaza kuwa, vitambulisho walivyopatiwa watu wa jamii ya walio wachache ya Rohingya muhula wake unamalizika mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu. Uamuzi huo wa serikali ya Myanmar unakinzana na hatua yake ya hapo awali ambapo ilitangaza kuwa, vitambulisho hivyo vitawaruhusu wenye navyo kupiga kura katika zoezi la kura ijayo ya maoni kuhusu katiba. Uamuzi huo wa serikali ya Myanmar umetangazwa masaa machache tu baada ya kundi la wananchi kuandamana katika mji mkuu Naypyidaw wakipinga Waislamu wa Rohingya kupiga kura katika uchaguzi.

Taarifa zaidi zinasema, makumi ya Mabudha walikuwa wakiongoza maandamano hayo. Serikali ya Myanmar haiwatambui Waislamu walio wachache wa kabila la Rohingya ambao ni zaidi ya watu milioni moja kuwa ni raia wa nchi hiyo. Serikali ya Myamnar inawatambua Waislamu wa Rohingya kuwa ni wahajiri haramu kutoka nchi jirani ya Bangladesh na imekuwa ikikataa kuwapatia uraia kamili. Serikali ya Myanmar imekuwa ikikosolewa na mashirika ya haki za binadamu kwa kushindwa kuwalinda Waislamu wa Rohingya wanaokabiliwa na unyanyasaji na mauaji yanayofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali. Maelfu ya Waislamu wameuawa nchini Myanmar na wengine wengi wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na hujuma hizo.../mh

2844150

captcha