IQNA

Wakimbizi

Bangladesh: Moto Waharibu Zaidi ya Makao 1,000 katika Kambi ya Wakimbizi ya Rohingya

20:22 - January 07, 2024
Habari ID: 3478161
IQNA - Moto ulikumba kambi ya wakimbizi wa Rohingya iliyojaa watu huko Cox's Bazar, wilaya ya pwani ya kusini mwa Bangladesh, Jumamosi usiku, na kuharibu zaidi ya makao 1,000 na kuwalazimu maelfu ya wakimbizi kuyahama makazi yao, kulingana na afisa wa zima moto na Umoja wa Mataifa.

Bangladesh: Moto Waharibu Zaidi ya Makao 1,000 katika Kambi ya Wakimbizi ya Rohingya

IQNA - Moto ulikumba kambi ya wakimbizi wa Rohingya iliyojaa watu huko Cox's Bazar, wilaya ya pwani ya kusini mwa Bangladesh, Jumamosi usiku, na kuharibu zaidi ya makao 1,000 na kuwalazimu maelfu ya wakimbizi kuyahama makazi yao, kulingana na afisa wa zima moto na Umoja wa Mataifa.

Moto huo ulizuka usiku wa manane katika kambi ya Kutupalong huko Ukhiya na kuenea haraka, ukiendeshwa na upepo mkali, alisema Shafiqul Islam, mkuu wa Kituo cha Zimamoto cha Ukhiya. Amesema kuwa hakuna aliyepoteza maisha au kujeruhiwa.

"Ulikuwa moto mkubwa, na uliteketeza takriban makazi 1,040 katika kambi hiyo," alisema. "Tulichukua takriban saa mbili kuzima moto huo, kwa msaada wa vitengo 10 vya zima moto kutoka Ukhiya na vituo vingine wilayani humo."

Maelfu ya wakimbizi, wakiwemo wanawake na watoto, wamekimbilia kwenye uwanja wazi wa karibu na mali zao huku moto ukiendelea asubuhi ya Jumapili.

"Tunasumbuliwa na baridi kali, tunakabiliwa na hali ngumu," alisema Zuhura Begum (65) ambaye alikuwa ameketi na wajukuu zake baada ya kutoroka moto, "Nyumba zetu zimeharibiwa."

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, limesema kwamba wafanyakazi wa kujitolea wa kukabiliana na moto walishirikiana na wazima moto kudhibiti moto huo. Ilisema tathmini ya kiwango cha uharibifu ilikuwa ikifanywa.

Chanzo cha moto huo hakijafahamika mara moja, lakini Islam ilisema taarifa za awali kutoka kwa wakimbizi hao zilidokeza kuwa moto huo ulianza kutoka kwenye tanuri ya udongo.

Moto ni wa kawaida katika kambi za wakimbizi Bangladesh, ambapo zaidi ya Waislamu milioni moja wa Rohingya wanaishi katika makazi duni na dhaifu. Mnamo Machi, moto uliacha maelfu ya wakimbizi bila makazi kwa muda.

Wakimbizi wengi walikimbilia Bangladesh kutoka Myanmar mwishoni mwa Agosti 2017, wakati jeshi la Myanmar lilishirikiana na Mabudhaa, wenye misimamo mikali ya chuki, lilipoanza ukandamizaji wa kikatili dhidi ya Rohingya. Waislamu hao Warohingya wamenyimwa uraia na haki nyingine za kimsingi nchini Myanmar, ambapo wanakabiliwa na ubaguzi na ukatili mkubwa.

Hali nchini Myanmar imezorota zaidi tangu mapinduzi ya kijeshi mwaka 2021, na juhudi za kuwarejesha makwao wakimbizi zimekwama. Waziri Mkuu Sheikh Hasina wa Bangladesh amekuwa akisema mara kwa mara kwamba wakimbizi hao hawatalazimishwa kurejea. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema hali nchini Myanmar si salama..

3486719

Kishikizo: bangaldesh rohingya
captcha