IQNA

Waziri wa Utawala wa Kizayuni wa Israel ataka viongozi wa Hamas watekwe nyara

20:02 - July 08, 2016
Habari ID: 3470439
Waziri mmoja katika utawala wa Kizayuni wa Israel ametaka viongozi wa ngazi za juu wa Hamas watekwe nyara.

Waziri wa elimu wa utawala haramu wa Israel Naftali Bennett amesema viongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, watekwe nyara ili watumiwe kuwalazimu Wapalestina walegeze misimamo katika mazungumzo. Amesema viongozi hao wa Hamas wakitekwa nyara watatumika kuishinikiza harakati hiyo kuachilia miili ya Waisraeli inayoshikiliwa katika Ukanda wa Ghaza.

Hamas imekiri kuwa inashikilia wanajeshi wanne wa utawala haramu wa Israel ambao walitekwa nyara wakati wa hujuma ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina aktika Ukanda wa Ghaza mwaka 2014.

Huko nyuma pia Bennett aliwahi kusema Israel inapaswa kuwateka nyara maafisa wa serikali ya Syria ili watumike kuilazimi serikali ya Syria ilegeze misimamo katika mazungumzo.

Bennett alikuwa afisa wa kikosi cha Sayeret Maktal cha makomando wa utawala wa Kizayuni ambao waliwateka nyara shakhsia wawili wa Lebanon, Abdel Karim Obeid mwaka 1989 na Mustafa Dirani 1994. Tel Aviv ilitumia mateka hao wawili kushinikiza Hizbullah kuachilia huru robani wa Kizayuni Ron Arad.

Kwa miaka mingi, Israel ambayo inaaminika kuwateka wanadiplomasia wanne Wairani nchini Lebanon, ilikuwa inadai kuwa eti Iran ilikuwa ikimshikilia Arad. Wanadiplomasia hao wanne Wairani walitekwa nyara Julai mwaka 1982, wakati wa hujuma ya Israel dhidi ya nchi hiyo.

Iran inasema wanadiplomasia hao walitekwa nyara na wanamgambo wa Phalange na kisha kuwakabidhi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika kumbukumbu ya mwaka wa 34 wa kutekwa nyara wanadiplomasia hao, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilisema ina ushahidi kuwa wanadiplomasia hao wanne waliotekwa nyara wako hai katika magereza ya Israel.

Mapema wiki hii mbunge mmoja wa Iran alisema Israel imetnagaza kuwa tayari kufanya mazungumzo na Hizbullah ambapo kadhia ya kurejeshwa wanadiplomasia hao itajadiliwa.

Javad Karimi Qoddousi aliliambia Shirika la Habari la Fars Jumanne wiki hii kuwa Israel iliitumia Hizbullah ujumbe na kutangaza kuwa tayari kujadili kadhia ya wanadiplomasia Wairani. Wanadiplomasia hao wanatazamiwa kubadilishwa na 'mateka wa kivita wneye uraia wa Ulaya' ambao walikamatwa wakipigana bega kwa bega na magaidi katiak mji wa Aleppo nchini Syria.

Kuna taarifa kuwa Hizbullah imewakamata maafisa wa kijasusi wa Marekani na Ufaransa kaskazini mwa Syria mwezi Mei huko Aleppo. Mbunge huyo amesema, adui yuko tayari kufanya mazungumzo kwa sababu majasusi waliotekwa nyara Syria wana thamani kubwa kwao. Qoddousi ambaye ni mwanachama wa Tume ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni katika Bunge la Iran amesema kiongozi wa Hizbullah Sayyed Hassan Nasrallah ameahidi kufuatilia kadhia hiyo binafsi.

3460328

captcha