IQNA

Iran yataka Umoja wa Mataifa ulaani mauaji ya Qassem Soleimani

20:47 - January 02, 2022
Habari ID: 3474756
TEHRAN (IQNA)- Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lipitishe azimio la kulaani kitendo cha Marekani cha kumuua kamanda wa Iran aliyeongoza vita dhidi ya ugaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani ili kwa njia hiyo kulinda amani na kimataifa na haki za binadamu.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Jumamosi na Kitengo cha Masuala ya Kisheria katika Ofisi ya Rais wa Iran ambayo imetolewa kwa munasaba wa mwaka wa pili wa mauaji ya kigaidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani mjini Baghdad.

Taarifa hiyo imesema rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alitangaza hadharini kuwa ndiye aliyeamuru jinai hiyo.  “Hatua hii hatari ya serikali ya Marekani imekuja katika hali ambayo Hati ya Umoja wa Mataifa inazuia serikali kujihusisha na vitendo ambavyo vinaweza kuhatarisha amani na usalama wa kimataifa.”

Aidha taarifa hiyo imekosoa kimya cha jamii ya kimataifa wakati Marekani inapokiuka sheria za kimataifa kupitia hatua zake za upande mmoja.

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, ambaye Januari 3 mwaka 2020 alielekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo aliuliwa shahidi akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq cha Hashd al Sha'abi na wanajihadi wengine wanane katika shambulio la kigaidi la jeshi la kigaidi la Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. Hujuma hiyo ilitekelezwa kufuatia amri ya rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump.

Kufuatia jinai hiyo, mnamo Januari 8 mwaka 2020, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilichukua hatua ya kulipiza kisasi kwa kuvurumisha makombora kadhaa dhidi ya kituo cha kijeshi cha Marekani cha Ain al Assad nchin Iraq.  Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa bado haijamaliza kulipiza kisasi mauaji ya Shahidi Soleimani na kwamba kuondoka askari wote wa Marekani katika eneo ndiko kutalipiza kisasi damu ya Luteni Jenerali Soleimani.

673851

captcha