IQNA

Hujuma dhidi ya Msikiti Peshawar yaendelea kulaaniwa

16:36 - March 07, 2022
Habari ID: 3475018
TEHRAN (IQNA)- Shambulio la kigaidi lililolenga Msikiti wa Waislamu wa Kishia mjini Peshawar Pakistan linaendelea kulaaniwa na pande mbalimbali ulimwenguni.

Shambulizi hilo lililofanywa na genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) lilitokea juzi Ijumaa wakati Waislamu walipokuwa Msikitini na liliua shahidi Waislamu 62 na kujeruhi wengine wapatao 200, wakubwa kwa wadogo.

Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan amelaani shambulio hilo la kigaidi lililowalenga Waislamu wa Kishia ndani ya Sala. 

Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran naye amelaani vikali jinai hiyo na kusema kuwa, lengo la magaidi hao ni kuzusha vita vikubwa katika safu za Waislamu.

Baraza la Maulamaa wa Kishia nchini Afghanistan pia limelaani shambulizi hilo la kigaidi dhidi ya Waislamu hao waliokuwa kwenye Sala ya Ijumaa huko Peshawar Pakistan na kuwataka Waislamu waungane kupambana na janga hili kubwa lililopandikizwa ndani ya umma wa Kiislamu ili kuipaka matope dini hii tukufu ya Allah ambayo msingi wake mkubwa ni rehema kwa viumbe wote. Baraza la Maulamaa wa Kishia la Afghanistan limesema kuwa, magenge ya kigaidi yanayofanya jinai hizo yanatumiwa na mashirika ya kijasusi ya madola ya kibeberu ili kuzusha mizozo na kuhakikisha Waislamu wa madhehebu mbalimbali hawakurubiani kivyovyote vile. 

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC nayo imelaani shambulio hilo lililofanya na magaidi wa ISIS dhidi ya Waislamu wa Kishia ndani ya Msikiti huko Peshawar Pakistan.

Mara kwa mara magaidi wa Daesh nchini Pakistan wamekuwa wakifanya mashambulizi ya kinyama na kikatili dhidi ya Waislamu wa Kishia na mbali na kuua kidhulma watu wasio na hatia, lengo lao jingine kuu ni kuzusha vita vikubwa vya kidini na kimadhehebu nchini Pakistan.

Tab'an si magaidi wa ISIS peke yao wanaoua kidhulma Waislamu wa Kishia nchini Pakistan. Katika miaka ya hivi karibuni, magenge mengine ya kigaidi kama lile la Sipah-e-Sahaba na Lashkar-e-Jhangvi yameshiriki katika mauaji ya Waislamu wasio na hatia wa Kishia.

Ijapokuwa magenge yote hayo yamepigwa marufuku nchini Pakistan, lakini yanaendelea kufanya jinai na mauaji ya kigaidi dhidi ya Waislamu na hadi hivi sasa mashirika na taasisi za kiusalama na kijasusi za Pakistan hazijachukua hatua yoyote kubwa ya kuhakikisha jinai hizo hazitendeki tena.

Jinai dhidi ya binadamu zinazofanywa na magaidi wa Daesh haziishii tu nchini Pakistan. Mwezi Oktoba 2021 magaidi hao walifanya mashambulizi ya kikatili dhidi ya Waislamu wa Kishia kwenye Sala mbili tofauti za Ijumaa katika mikoa ya Kunduz na Kandahar nchini Afghanistan na kuua shahidi na kujeruhi mamia ya Waislamu. Mashambulio hayo yaliliweka chini ya mashinikizo makubwa kundi la Taliban lililotwaa madaraka ya Afghanistan na kutakiwa kulipa uzito mkubwa suala la kuwalinda Waislamu wanapokuwa Misikitini.

Kwa kutilia maana kwamba genge la kigaidi la Daesh ni adui wa pamoja wa nchi zote za eneo hili zikiwemo Pakistan na Afghanistan, kinachotarajiwa ni kuona nchi hizo mbili zinaweka pembeni hitilafu zao na kuunganisha nguvu zao kwa ajili ya kupambana vilivyo kwa pamoja na janga hilo la genge la ISIS na magenge mengine ya kigaidi.

Kwa kuzingatia kuwa, nchi mbalimbali ni wahanga wa vitendo vya kigaidi vya Daesh katika maeneo tofauti duniani, dunia nzima inapaswa kutambua kuwa, maadamu hakuna mtazamo mmoja kieneo na kimataifa juu wa wajibu wa kupambana vilivyo na magenge kama hayo ya kigaidi, tusitaraji kabisa kubadilika hali iliyopo hivi sasa na tusiwe na tamaa kabisa kwamba kuna siku walimwengu wataweza kuishi bila ya wasiwasi wa kukumbwa na mashambulio ya magenge ya kigaidi kama ISIS.

3478068

 

captcha