IQNA

Magaidi washambulia shule katika mji wa Kabul, Afghanistan

17:27 - April 19, 2022
Habari ID: 3475141
TEHRAN (IQNA)- Wanafunzi zaidi ya 27 wameuawa kufuatia hujuma ya kigaidi katika shule moja ya wavulana katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul Jumanne.

Taarifa zinasema magaidi waliokuwa wamesheheni mabomu wameshambulia Shule ya Abdul Rahim Shahid iliyopo katika mtaa wa Dashte Barchi ambao wakaazi wake wengi ni Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Imedokezwa kuwa gaidi wa kwanza alijilipua  wakati wanafunzi walipokuwa wakiondoka shuleni baada ya kumalizika masomo ya asubuhi na baada ya muda usio mrefu gaidi wa pili akajilipua wakati waalimu walipokuwa wakijaribu kuwasaidia waliokuwa wamejeruhiwa katika mlipuko wa kwanza. 

Asubuhi ya leo pia mllipuko mwingine uliripotiwa katika Shule ya Mumtaz katika eneo hilo hilo la Dashte Barchi. Hakuna watu walioripotiwa kupoteza maisha katika mlipuko uliolenga shule hii ya pili.

Milipuko ya leo imejiri wiki mbili kabla ya kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa hujuma ya bomu dhidi ya Shule ya Upili ya Sayed Ul-Shuhada ambapo wanafunzi 90, wengi wakiwa ni wasichana waliuawa.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afghanistan imeamuru uchunguzi ufanyike kuhusu hujuma hiyo ya kigaidi. Hadi sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi hilo lakini weledi wa mambo wanaamini kuwa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh ndilo lililohusika. Kundi la ISIS limedai kuhusika na mashambulizi kadhaa dhidi ya maeneo ya Mashia mjini Kabul.

4050792

captcha