IQNA

Hujuma ya kigaidi dhidi ya Msikiti wa Waislamu wa Kishia Afghanistan yalaaniwa

21:47 - April 22, 2022
Habari ID: 3475155
TEHRAN (IQNA)- Umoja wa Mataifa umelaani mlipuko wa kigaidi uliotokea karibuni katika msikiti wa Waislamu wa Kishia huko Mazar-Sharif katika mkoa wa Balkh, Afghanistan.

Mlipuko wa kigaidi uliotokea Alhamisi adhuhuri katika Msikiti wa Seh Dokan huko Mazar-Sharif; ambao ni msikiti mkubwa na mkongwe zaidi wa Waislamu wa Kishia katikati ya mji huo kaskazini mwa Afghanistan umeua makumi ya waumini  na kujeruhi wengine kadhaa.

Mbali na mlipuko huo wa kigaidi, majimbo mengine matatu huko Afghanistan jana yalikumbwa na milipuko kadhaa ya umwagaji damu. Jinai zote hizo zimejiri wakati wa Swala ya Adhuhuri jana Alhamisi. Umoja wa Mataifa umetoa taarifa na kulaani mlipuko huo wa kigaidi uliotekelezwa katika Msikiti wa Waislamu wa Kishia huko Mazar-Sharif.

Stephane Dujaric msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa Ofisi ya Uwakilishi ya umoja huo huko Afghanistan imelaani hujuma hiyo ya kigaidi. Dujaric amebainisha wasiwasi wake kuhusu mashambulizi yanayotekelezwa kuwalenga raia huko Afghanistan na ametaka kusitishwa hujuma hizo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Saeed Khatibzadeh amelaani hujuma hizo na kusema Iran ina wasiwasi kuhusu matukio hayo ya kusikitisha.

Aidha amesema ni jambo la kuchukiza kuona magaidi wanatekeleza hujuma hizo katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani dhidi ya Waislamu walio katika saumu ndani ya misikiti.

Naye msemaji wa serikali ya Afghanistan Zabihullah Mujahid amelaani vikali hujuma hizo za kigaidi dhidi ya maeneo ya waislamu wa madhehebu ya Shia. Amesema vitendo kama hivyo havihusiana hata kidogo na jamii ya watu wa Afghanistan.

Ameongeza kuwa serikali ya Taliban nchini Afghanistan ina uzoefu wa kuangamiza makundi ya kigaidi na kuongeza kuwa wahusika watatiwa mbaroni na kuwajibishwa. 

Nayo harakati ya Hizbullah ya Lebanon imelaani vikali hujuma dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Afghanistan na imetaka serikali za Kiislamu duniani kulaani ugaidi huo wa wakufurishaji.

Kundi la kitakfiri na kigaidi la Daesh (ISIS) limetangaza kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi katika Msikiti wa Mazar-Sharif. Wakati huo huo televisheni ya al Mayadeen imetangaza kuwa, hadi sasa watu 40 wameuliwa shahidi na 100 kujeruhiwa katika hujuma hiyo ya kigaidi huko Mazar-Sharif. 

3478594

captcha