IQNA

Umoja wa Kiislamu

Iran imeandaa Kongamano la 36 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu

19:57 - October 08, 2022
Habari ID: 3475898
TEHRAN (IQNA)- Kongamano la 36 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu litafanyika mjini Tehran kuanzia tarehe 17 hadi 22 Oktoba kwa kuhudhuriwa na wasomi na wanafikra kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Mkutano huo umeandaliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu na unatazamiwa kuhudhuriwa na wasomi na wanafikra kutoka sehemu mbalimbali za dunia, ambapo mada muhimu zitajazojadiliwa ni pamoja na: udugu wa Kiislamu na mapambano dhidi ya ugaidi, uhuru wa kidini, kukubali ijtihadi ya Kiislaamu na kukabiliana na fikra za ukufurishaji na misimamo mikali, kuheshimiana baina ya madhehebu  Kiislamu, kuzingatia adabu wakati kunapokuwepo tofauti na kuepuka malumbano, mivutano, mizozo, dharau na matusi, kuzingatia huruma ya Kiislamu na huruma na kuepukana na kupinga uanzishwaji wa uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni.

Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu imekuwa ikiandaa kongamano la kimataifa la Umoja wa Kiislamu kila mwaka kwa muda wa miaka 35 sasa.

Kongamano hilo kwa kawaida hufanyika Tehran, mji mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Tuko katika siku tukufu za kuadhimisha Maulid ya Mtume Mtukufu wa Uislamu Mohammad al Mustafa SAW, siku ambazo ni maarufu kama siku za Maulidi. Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanaadhimisha siku hiyo tarehe 12 Rabiul Awwal na Waislamu wa Madhehebu ya Shia wanamini siku hiyo ni tarehe 17 Rabiul Awwal.

Miaka mingi iliyopita, Hayati Imam Khomeini MA, Kiongozi mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambaye binafsi alikuwa mstari wa mbele kulingania umoja wa Kiislamu alipendekeza kuwa, muda uliopo baina ya tarehe hizo mbili uwe ni "Wiki ya Umoja wa Waislamu" kwa lengo la kuimarisha mashikamano na udugu baina ya madhehebu za Kiislamu.

4090395

captcha