IQNA

Jinai za Israel

Baraza la Usalama lataka kudumishwa hali ya sasa ya Msikiti wa Al Aqsa

13:55 - January 06, 2023
Habari ID: 3476366
TEHRAN (IQNA)-Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamesisitiza juu ya ulazima wa kudumisha hali ya miongo kadhaa iliyopita katika eneo la Msikiti wa al-Aqsa katika Mji Mkongwe wa al-Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala wa Israel baada ya utawala huo ghasibu kulivunjia heshima eneo hilo takatifu.

Tamko hilo la Baraza la Usalama  limekuja kwa kuchelewa siku ya Alhamisi baada ya waziri mwenye mitazamo mikali ya mrengo wa kulia wa Israel Itamar Ben-Gvir kuchukkua hatua yenye utata ya kuuvunjia heshima Msikiti wa al-Aqsa. Kitendo hicho cha kichokozi kiliwakasirisha Wapalestina na Waislamu kote duniani kwani wanaoruhusiwa kufanya ibada katika msikiti huo mtakatifu ni Waislamu pekee.

Baraza hilo lenye wajumbe 15 lilijadili kuhusu hujuma hiyo ya Israel dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa kufuatia ombi la Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na China. Katika hikao hicho  mjumbe wa Palestina na mwakilishi wa utawala ghasibu wa Israel walirushiana maneneo makali kuhusu uchokozi huo wa kuuvunjia heshima Msikiti wa Al Aqsa.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa wa Palestina Riyad Mansour alisema vitendo vya Israel ni vya "dharau kabisa," huku akilitaka Baraza la Usalama kuchukua hatua dhidi ya utawala huo haramu, akisisitiza, "Ni mstari gani mwekundu ambao Israel inahitaji kuvuka ili Baraza la Usalama liseme, inatosha?"

Afisa mkuu wa masuala ya kisiasa wa Umoja wa Mataifa, Khaled Khiari, ameliambia baraza hilo lenye wanachama 15 kuwa ni hujuma ya kwanza ya waziri wa Israel katika eneo hilo takatifu tokea mwaka 2017.

Khiari ameseme kitendo cha waziri huyo wa Israel cha kuvunjia heshima Msikiti wa Al Aqsa ni cha kichochezi haswa kutokana na kauli za hapo awali za Ben-Gvir kuwa kunapaswa kuwa na mabadiliko katika matumizi ya Msikiti wa Al Aqsa.

Robert Wood, naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, ameliambia baraza hilo kwamba Washington "inasikitishwa na vitendo vyovyote vya upande mmoja vinavyozidisha mivutano," na kutoa wito wa "kuhifadhiwa kwa hali iliyopo kuhusiana na maeneo matakatifu."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia amezitaka pande hizo mbili kujiepusha na hatua zinazoweza kuzidisha mivutano ndani na karibu na maeneo matakatifu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Baada ya kikao hicho cha saa mbili kukamilika, Mansour alionyesha kuridhishwa na kile alichokiita "umoja wa Baraza la Usalama katika kutetea hali iliyopo," akiongeza kuwa hatarajii hatua zaidi madhubuti kutoka kwa chombo hicho cha kimataifa.

Gilad Erdan, balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, amekiita kikao hicho cha "upuuzi" na kusema "hakukuwepo sababu kabisa" ya mkutano huo kufanyika.

Jumanne iliyopita waziri  huyo wa Israel aliingia katika Msikiti wa Al Aqsa na kuuvunjia heshima, kitendo ambacho kimeibua wimbi la kulaaniwa kimataifa, ikiwemo kutoka Marekani, mshirika wa muda mrefu wa utawala huo ghasibu, pamoja na mamlaka za Palestina na ulimwengu wa Kiislamu.

Kufuatia kitendo hicho cha uhalifu, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amewatahadharisha viongozi wa nchi za Kiislamu kuhusuu njama za kila namna za serikali mpya ya kifashisti ya Israel na kuwataka waamke kuuokoa Msikiti wa Al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu.

Ismail Haniya ametoa tahadhari hiyo Jumatano na kuzitaka nchi za Kisilamu na Kiarabu kuchukua misimamo imara na ya wazi kukabiliana na njama za utawala wa Kizayuni wa Israel. 

3481966

captcha