IQNA

Jinai za Israel

Serikali katili ya Marekani yatumia kura ya turufu kuzuia usitishaji vita Gaza

15:11 - December 09, 2023
Habari ID: 3478009
NEW YORK (IQNA)- Marekani, ambayo ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, imetumia kura yake ya turufu kupinga azimio lililopendekezwa na UAE la kuanzisha usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza.

Muswada huo umepigiwa kura katika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama uliofanyika usiku wa kuamkia leo, na kupasishwa na wanachama 13 kati ya 15 wa baraza hilo. Marekani imeupinga kwa kura ya turufu au veto huku Uingereza ikijizuia kupiga kura. Muswada huo ulitoa wito wa "kusitishwa mapigano mara moja kwa sababu za kibinadamu" na kuungwa mkono na nchi za Kiarabu na Kiislamu.

Azimio lolote linahitaji kwa uchache kura 9 ili kupasishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa bila kupingwa kwa kura ya veto ya wajumbe 5 wa kudumu wa baraza hilo yaani Marekani, Uingereza, Ufaransa, Russia na China.  Mkutano huo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ulifanyika baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kutumia Ibara ya 99 ya Hati ya Umoja wa Mataifa, ambayo ni nadra sana kutumiwa na Katibu Mkuu wa umoja huo, akilitolea wito Baraza la Usalama "kushinikiza kuepusha janga la kibinadamu" katika Ukanda wa Gaza kutokana na maafa makubwa yanayosababishwa na mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa neo hilo. Hii ni mara ya kwanza kwa Guterres kufanya hivyo tangu achaguliwe kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, mwaka 2017.

Dunia hatarini

Ibara ya 99 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambayo imetumika mara 9 pekee katika historia ya umoja huo, inamruhusu Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo kubwa zaidi duniani kuwaita wajumbe wa Baraza la Usalama kwenye mkutano wa dharura wakati anapohisi kwamba "amani na usalama wa dunia" uko hatarini na kuwataka wachukue hatua za haraka kuhusu suala hilo. 

Baada ya hatua hiyo, jana Ijumaa kulifanyika kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali ya Gaza kilichohudhuriwa na Guterres, na nchi mbalimbali zilitoa maoni yao juu ya kadhia hiyo. Hata hivyo, balozi wa Marekani ambayo ni mojawapo ya wanachama 5 wa kudumu wa Baraza la Usalama, hadi usiku wa kuamkia mkutano huo, alijizuia kutoa maoni yake ya wazi kuhusu hatua hiyo ya Katibu Mkuu wa UN, na hatimaye nchi hiyo ilipinga azimio lililopendekezwa la kusitishwa mara moja mapigano huko Gaza.

Baraza la Usalama limeshindwa

Antonio Guterres aliamua kutumia Ibara ya 99 ya Hati ya Umoja wa Mataifa baada ya hali ya watu wa Gaza kuwa mbaya sana kutokana na mauaji yanayoendelea kufanywa na Israel katika eneo hilo la Palestina. Takwimu zinaonyesha kuwa, karibu Wapalestina elfu 20, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake, wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 42,000 wamejeruhiwa kutokana na mashambulizi ya kikatili ya Israel. Idadi kubwa ya raia inaendelea kuuawa kila siku na misaada ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na chakula, dawa na maji, haiwezi kupelekwa Gaza kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel. Haya yote yanaonyesha jinsi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilivyoshindwa kutekeleza majukumu yake ya kudumisha amani na usalama wa kimataifa na kumaliza migogoro ya kikanda.

Vilevile inaonekana kuwa, itakuwa vigumu sana kufikia maoni ya pamoja kuhusu vita vya Gaza, kwa kuzingatia haki ya kura ya veto ya wanachama 5 wa kudumu wa baraza hilo, yaani Marekani, Uingereza, Ufaransa, Russia na Uchina.

Marekani ni muungaji mkono wa jinai za Israel

Wakati huo huo, yaliyojiri jana katika Baraza la Usalama la UN yamedhirisha zaidi nafasi ya nchi za Magharibi wanachama wa Baraza la Usalama zinazoongozwa na Marekani katika kuendelea mauaji ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Gaza. Marekani, kama muungaji mkono mkuu wa Israel, imeipa Tel Aviv mwanga wa kijani wa kuendeleza mauaji na uharibifu katika eneo la Ukanda wa Gaza kwa kupiga kura ya veto dhidi ya maazimio yote yanayotoa wito wa kusitisha mapigano huko Gaza. Kwa hivyo, wakati hali ya Gaza imepita kiwango cha kuitwa "maafa ya binadamu" na inaelezwa kwa maneno kama "jahannamu ya duniani" na "hali ya akheri zamani", Marekani, kwa mara nyingine tena, imepinga rasimu ya azimio la Baraza la Usalama la kusitishwa vita mara moja huko Gaza na kuupa utawala wa Kizayuni fursa zaidi ya kufanya mauaji ya kimbari ya Wapalestina.

Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Gilad Erdan, mwakilishi wa kudumu wa utawala wa Israel katika Umoja wa Mataifa ameishukuru serikali ya Joe Biden kwa hatua yake katika Baraza la Usalama. Hata hivyo Dmitri Polyansky, naibu mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amekosoa hatua ya Marekani na kusema: "Washington, kwa mara nyingine imezuia usitishaji vita huko Gaza; na kuzuia usitishaji vita kuna maana ya hukumu ya kifo ya Marekani dhidi ya maelfu na pengine makumi ya maelfu ya watu wa Wapalestina." 

Habari zinazohusiana
captcha