IQNA

Umoja wa Waislamu

Mwanazuoni: Mungu Mmoja, Kitabu Kimoja, Nabii Mmoja ni nukta za kuwaunganisha Waislamu

18:18 - October 07, 2023
Habari ID: 3477695
TEHRAN (IQNA) – Mwanazuoni wa Kiislamu kutoka Madagaska amesisitiza haja ya kuzingatia nukta za pamoja kwa ajili ya kujenga umoja kati ya Waislamu.

Akizungumza na IQNA kando ya Kongamano la 37 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu ambalo limefanyika hivi karibuni kwa mnasaba wa Maulid ya Mtume Muhammad (SAW) na Wiki ya Umoja wa Kiislamu, mkuu wa kituo cha utamaduni cha Al-Ghazali nchini Madagascar Abdourazak Ali Mahomad amezungumzia haja ya kujenga umoja baina ya Waislamu duniani kote.

Ikizingatiwa kuwa mataifa ya Kiislamu yamekuwa yakilengwa na nchi za Ulaya na Marekani katika kipindi cha miaka 300 iliyopita, mataifa ya Kiislamu lazima yazingatie zaidi umoja wa Kiislamu kwa sababu hii inaweza kuwa na jukumu kubwa katika mustakabali wao, alisema.

"Kwa bahati mbaya, baadhi ya watu wanajaribu kuleta mgawanyiko kwa kuendeleza masuala kuibua migongano baina ya wafuasi wa madhehebu za Shia  na Sunni; naamini hili si sahihi," alisema.

“Sote ni wanajamii moja na tunaamini katika Mungu Mmoja, Kitabu Kimoja na Nabii mmoja na sote tunapaswa kujenga umoja kwa kuzingatia maadili yetu ya pamoja,” aliongeza.

Akipongeza kuanzishwa tena kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Iran na Saudi Arabia, alisema kuwa hilo linaweza kutokea baina ya mataifa mengine ya Kiislamu pia.

"Ikiwa tutakubali umoja, ninaamini mustakabali mwema unawangoja Waislamu kote ulimwenguni," alisema.

Ali Mahomad amebainisha kuwa uhusiano kati ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni nchini Madagaska ni mzuri kwani wanashirikiana katika masuala mbalimbali ya kijamii.

Mkutano wa 37 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu, uliofanyika ana kwa ana na mtandaoni, ulizinduliwa Tehran siku ya Jumapili.

Zaidi ya wasomi 200 wa Iran na nchi za nje na shakhsia wa kidini kutoka nchi mbalimbali za Kiislamu wanashiriki katika mkutano huo ambao umeandaliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha  Madhehebu za Kiislamu ambao ulimalizika  Oktoba 3.

Kongamano hilo hufanyika kila mwaka wakati wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu.

Siku ya 17 ya Rabi al-Awwal, ambayo inaangukia Oktoba 3 mwaka huu, inaaminika na Waislamu wa madhehebu ya Shia kuwa ni siku ya kuzaliwa kwa Mtume Mohammad (SAW), wakati Waislamu wa Sunni wanaichukulia siku ya 12 ya mwezi (Septemba 28) kama siku ya kuzaliwa. kwa nabii huyo wa mwisho.

Muda kati ya tarehe hizo mbili huadhimishwa kila mwaka kama Wiki ya Umoja wa Kiislamu.

Hayati Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Khomeini (RA) alitangaza maadhimisho hayo kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu mnamo 1980.

3485445

Kishikizo: umoja wa waislamu
captcha