IQNA

Mapambano ya Kiislamu (Muqawama Islamiya)

Kiongozi wa Hamas: Wapalestina wamishurutisha Israel kusitisha vita

20:28 - November 25, 2023
Habari ID: 3477942
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, amesema Wapalestina wameulazimisha utawala wa Kizayuni wa Israel kukubali masharti ya kundi hilo katika mapatano ya kusitisha mapigano huku akiapa kuwa wapiganaji wa Hamas wataendelea kupigania ukombozi wa Palestina.

Akizungumza siku ya Ijumaa, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas Ismail Haniyah amesema wapigania ukombozi au wanamuqawama waliweza kukabiliana na utawala vamizi wa Israel na kuvunja irada ya utawala huo sambamba na kuzuia mpango wake wa kuwakomboa mateka wake kupitia mauaji ya kimbari.

Kiongozi huyo wa Palestina amesema kundi hilo liko tayari kuendelea kukabiliana na mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza baada ya usitishaji mapigano wa siku nne ulioanza Jumanne.

Ameapa kwamba Hamas haitaacha wadhifa wake huko Gaza na amepinga vikali "uingiliaji wowote wa nje" kuhusu jinsi eneo hilo litakavyoendeshwa katika siku zijazo.

Katika hotuba yake, Haniyah amesema Hamas itazingatia mapatano ya kusitisha mapigano na kubadilishana wafungwa maadamu utawala wa Kizayuni utazingatia suala hilo.

Amesema Wapalestina wanapigana vita vya ukombozi wa taifa katika eneo la Gaza, al-Quds na maeneo mengine yote.

Jumla ya mateka 39 wa Kipalestina wa kike na watoto wameachiliwa huru na utawala wa Kizayuni wa Israel katika gereza la Ofer katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu huku usitishaji mapigano ukiendelea kwa muda katika Gaza kufuatia majuma sita ya mashambulizi ya Israel.

Wakati wa mapatano ya siku nne, wafungwa Wazayuni wasiopungua 50 wanatarajiwa kuachiliwa na wengine 190 watasalia huko Gaza. Aidha utawala haramu wa Israel unapaswa kuwaachilia huru mateka 150 wa Kipalestina, wote wanawake na wavulana matineja.

Vita vya mauaji ya kimbari vya utawala katili wa Israel dhidi ya Gaza vimesababisha vifo vya takriban Wapalestina 15,000, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.

Waziri wa vita wa Israel Benny Gantz amesema katika mkutano wa hadhara huko Tel Aviv kwamba utawala huo utaanzisha tena mapigano baada ya kumalizika muda wa usitishaji vita ulioanza Ijumaa asubuhi.

3486160

captcha