IQNA

Jinai za Israel

UNRWA yakosoa "Adhabu ya Pamoja' dhidi ya Wapalestina milioni mbili Gaza

17:03 - January 28, 2024
Habari ID: 3478265
IQNA - Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi la Palestina UNRWA amesema kuwa uamuzi wa baadhi ya nchi za Magharibi kusitisha misaada ya kifedha kwa shirika hilo ni sawa na "adhabu ya pamoja" ambayo itapunguza misaada ya kuokoa maisha kwa watu milioni mbili huko Gaza.

Philippe Lazzarini aliandika katika chapisho kwenye X, zamani Twitter siku ya Jumapili kwamba misaada ambayo UNRWA huwapa wakimbizi Wapalestina inakaribia kumalizika.

Aliendelea kuandika kuwa: "Operesheni yetu ya kibinadamu, ambayo watu milioni 2 wanategemea kama njia ya kuokoa maisha huko Gaza, inasambaratika. Ninashangaa maamuzi kama haya yanachukuliwa kwa mujibu wa mwennendo wa watu wachache  wakati vita vinaendelea, mahitaji yanazidi kuongezeka na njaa inanyemelea." Halikadhalika amesema "Wapalestina wa Gaza hawakuhitaji adhabu hii ya ziada ya pamoja. Hii inatutia doa sote.”

 UNRWA imetangaza kwamba inaanzisha uchunguzi baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kudai kuwa baadhi ya wafanyakazi wa shirika hilo walihusika katika operesheni ya tarehe 7 Oktoba ya Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya utawala huo ghasibu.

Tuhuma hizo zilizotolewa na utawala wa Kizayuni zimesababisha nchi zisizopungua 10 za Magharibi kujiondoa au kusitisha kwa muda misaada yao ya kifedha kwa shirika hilo la UN, hatua ambayo mkuu wa UNRWA amesema ni "ya kushtusha".

Lazzarini alisema katika taarifa yake Ijumaa alisema kulinda uwezo wa UNRWA wa kutoa msaada wa kibinadamu, nimechukua uamuzi wa kusitisha mara moja kandarasi za wafanyikazi hawa na kuanzisha uchunguzi ili kubaini ukweli bila kuchelewa,"  

Marekani ilitangaza Ijumaa kuwa inasitisha ufadhili kwa UNRWA kwa sababu ya madai ya Israel dhidi ya wafanyakazi 12 wa shirika hilo.

Kanada na Australia zilifuata mkumbo na kutangaza kusitisha ufadhili sawa na UNRWA ambayo ni chanzo muhimu cha msaada kwa watu wa Gaza.

Uingereza, Ujerumani, Italia, Uholanzi, Uswizi, Scotland na Finland siku ya Jumamosi zilijiunga na Marekani katika kusitisha ufadhili kwa shirika hilo la misaada.

Ireland na Norway, hata hivyo, zilionyesha kuendelea kuunga mkono UNRWA, zikisema shirika hilo linafanya kazi muhimu kuwasaidia Wapalestina waliokimbia makazi yao na wanaohitaji msaada mkubwa Gaza.

Kiongozi wa zamani wa upinzani nchini Uingereza, Jeremy Corbyn aliutaja uamuzi wa Uingereza kusimamisha msaada wa UNRWA kuwa ni kitendo cha "adhabu ya pamoja" dhidi ya watu wa Gaza.

Corbyn alisema katika chapisho kwenye X siku ya Jumamosi kwamba Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ0 ilisema Israel inapaswa kuchukua hatua za kusitisha mauaji ya kimbari Gaza. Leo, Uingereza imeungana na wengine katika kusimamisha ufadhili kwa UNRWA.

Siku ya Ijumaa, katika kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Israel kuhusu mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) inaamini kuwa kuna  "uwezekano" kwamba Israel imefanya vitendo vinavyokiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari.

3486989

Habari zinazohusiana
captcha