IQNA

Waislamu wa Myanmar wanyimwa haki ya Kuhiji kwa muongo moja sasa

16:58 - September 07, 2016
Habari ID: 3470551
Myanmar inaendeleza sera za kuwakandamiza Waislamu wa nchi hiyo na kwa mara nyingine mwaka huu imewazuia kwenda kutekeleza ibada tukufu ya Hija Waislamu ikiwa ni mwaka wa kumi mfululizo kufanya hivyo.

Kunyimwa makumi ya Waislamu wa Myanmar haki yao ya kwenda kutekeleza ibada tukufu ya Hija ni hatua ya karibuni kabisa ya uadui wa serikali inayodai si ya kijeshi ya Myanmar. Bila ya shaka ni watu wachache mno wanaoshindwa kuunganisha moja kwa moja ukatili wa serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu kila linapotajwa jina la nchi hiyo inayotawaliwa kidikteta na mabudha.

Bi Aung San Suu Kyi, ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Myanmar ambaye pia ni mshauri mkuu wa serikali na ratiba nyingi za serikali hiyo zinaendeshwa kwa ushauri wake. Hivyo ni jambo lisilo na shaka kabisa kwamba waziri huyo ana mkono wa moja kwa moja katika hatua zinazochukuliwa na serikali ya mabudha ya nchi hiyo. Ikumbukwe kwamba, hivi karibuni kulikuwa na mkutano wa siku nne wa suluhu baina ya makundi na kaumu mbalimbali za Myanmar lakini Waislamu hawakualikwa kwenye mkuktano huo. Ijapokuwa Ban Ki moon alilalamikia kutoshirikishwa Waislamu kwenye mkutano huo muhimu wa kuainisha mustakbali wa nchi hiyo, lakini maneno matupu hayawezi kuwasaidia chochote Waislamu wanaokandamizwa kinyama huko Myanmar.

Kwa kweli siasa kuu za serikali ya Myanmar ni kutowatambua Waislamu wa kabila la Rohingya, bali hawawapi hata haki ya kuishi kwa salama kama wageni. Wanawahesabu Waislamu kuwa ni watu wasio na utambulisho wa aina yoyote ile. Ijapokuwa Umoja wa mataifa, Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC na baadhi ya taasisi za kijamii zimefanya jitihada kubwa katika miaka ya hivi karibuni ili kuishawishi serikali ya Myanmar iwatambue Waislamu hao kuwa ni katika jamii ya wachache ya nchi hiyo, lakini jitihada hizo hazijafanikiwa hadi hivi sasa.

Wataalamu wa masuala ya Hija wanasema kuwa, suala la kwenda mahujaji katika miji mitakatifu ya Makka na Madina lina masharti na njia zake, si kwamba kila mtu anaweza kujiendea Hija tu bila ya utaratibu maalumu kama vile kuwa na pasi ya kusafiria, viza na kujulikana uraia wake na nchi anayotoka. Hata hivyo serikali ya Myanmar inawanyima Waislamu hao haki zao hizo za kimsingi, na hivyo inawazuia kwenda kutekeleza ibada hiyo tukufu. Hata hivyo wachambuzi hao wa mambo wanasema, kabla ya kulaumiwa mabudha wa Myanmar, tujikumbushe kwanza kwamba Waislamu wa Myanmar si peke yao wanaozuiwa kwenda kutekeleza amali ya Hija.

Utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Saud wa nchini Saudi Arabia unatumia ibada ya Hija kwa malengo ya kisiasa na unawazuia Waislamu wa nchi mbalimbali kama vile Syria, Yemen na Iran kwenda kutekeleza ibada hiyo muhimu. Kitendo cha mabudha wa Myanmar cha kuwazuia Waislamu kwenda kutekeleza ibada ya Hija hakikubaliki hata kidogo, lakini inaonekana kuwa mabudha hao nao wanatumia wenzo huo huo wa siasa kuwazuia Waislamu wa nchi hiyo kwenda Hija.

Alaakullihaal! Jitihada mbalimbali zinafanyika kuhakikisha kuwa Waislamu wa Myanmar wanatambuliwa rasmi na kupata haki zao za kisheria ikiwemo haki ya kutekeleza ibada tukufu ya Hija. Mkurugenzi wa kituo cha upashaji habari cha Waislamu wa Rohingya Bw,. Salah Abdul Shakur amesema wameanzisha harakati mbalimbali za kukabiliana na unyanyasaji wanaofanyiwa Waislamu wa Myanmar kama njia ya kutangaza mateso yao kwa walimwengu na kuonesha namna serikali ya Myanmar inavyokanyaga bila huruma, haki za Waislamu hao.

3527952


captcha