IQNA

Afisa wa Umoja wa Mataifa

Waislamu wa Myanmar wanaishi katika hali mbaya sana

19:33 - October 16, 2016
Habari ID: 3470615
Afisa wa ngazi za juu katika Umoja wa Mataifa amesema Waislamu Zaidi ya 120,000 nchini Myanmar wanaishi katika hali mbaya sana wakiwa katika kambi za wakimbizi wa ndani ya nchi.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Stephen O'Brien, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kibinadamu amesema kufuatia machafuko ya hivi karibuni katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar, Waislamu wanakabiliwa na hali mbaya na kunapaswa kuchukuliwa hatua za haraka kuwalinda na kuzuia machafuko Zaidi eneo hilo. Akizungumza baada ya safari yake ya siku tatu nchini Myanmar iliyomalizika Ijumaa, O'Brien amesema ameshuhudia kwa macho yake hali mbaya ya Waislamu ambao wanaishi kwa umasikini mkubwa huku wakiteswa na wakinymwa haki zao na utawala wa Myanmar.

Shambulio la hivi karibuni la watu wasiofahamika katika kituo cha ulinzi wa mpakani kati ya Myanmar na Bangladesh kimekuwa kisingizio tosha kwa jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali huko Myanmar cha kuwashambulia tena Waislamu wa Rohingya katika mkoa wa Rakhine.

Mabudha wanawakandamiza Waislamu

Viongozi wa kieneo na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada wamewatuhumu Waislamu wa Rohingya kuwa walihusika kwenye shambulio hilo ambapo askari tisa wa jeshi la Myanmar waliuawa, na hivyo kulishambulia eneo wanapoishi Waislamu hao na kuwaua watu zaidi ya ishirini miongoni mwao. Wakati huo huo maelfu ya Waislamu wa Rohingya wamezikimbia nyumba zao wakiepa mashambulizi ya wanajeshi na Mabudha wenye misimamo mikali.

Watu walioshudia wameeleza kuwa, Waislamu wengi wa Rohingya walioaga dunia waliuliwa kwa kupigwa risasi kutokea nyuma ambapo hakuna hata Mwislamu mmoja kati ya hao aliyekuwa na silaha. Waislamu wa Rohingya huko Myanmar wanaofikia milioni moja na laki tatu katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa chini ya mashinikizo makubwa, mateso na ukandamizaji wa serikali na makundi yenye misimamo mikali nchini humo.

Waislamu Myanmar wananyimwa uraia

Serikali ya Myanmar inaitambua kaumu ya Rohingya kuwa ni watu wenye asili ya Bangladesh na kwa msingi huo haiwezi kuwapa uraia wa Myanmar. Mabudha wenye misimamo ya kuchupa mipaka na baadhi ya mirengo ya kijeshi huko Myanmar wanatekeleza siasa za kuchoma ardhi lengo likiwa ni kuwafukuza majumbani mwao na kupora ardhi za Waislamu hao. Sababu hiyo imewafanya Waislamu wa Rhingya zaidi ya 150,000 kuishi kwa taabu na mashaka katika kambi za wakimbizi huko Myanmar na katika nchi nyingine jirani.

Kuuliwa ovyo jamii hiyo na upuuzaji unaofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu hao, yote hayo yameupelekea Umoja wa Mataifa kuwaarifisha Waislamu wa Rohingya kuwa ni kaumu ya wachache iliyodhulumika zaidi duniani.

Hata kama umoja huo, nchi na taasisi nyingi za kimataifa zimeitaka serikali ya Myanmar kushughulikia hali ya Waislamu wa Rohingya na kuzuia mashambulizi ya Mabudha wenye misimamo mikali dhidi ya jamii hiyo, hata hivyo serikali isiyo ya kijeshi ya Aung San Suu Kyi Kiongozi wa chama tawala cha The National League for Democracy pia haijachukua hatua yoyote ya maana kwa ajili ya kuwalinda Waislamu hao na kuwapatia haki zao za kiraia.

Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel anahusika kuwakandamiza Waislamu

Weledi wa masuala ya kisiasa wanaona kuwa kwa kuzingatia kuwa San Suu Kyi na chama tawala cha The National League for Democracy wana ushawishi miongoni mwa Mabudha wenye misimamo mikali, yeye bado ana wasiwasi wa kupoteza uungaji mkono wake kutoka chama tawala na sababu hiyo imemfanya Aung San Suu Kyi, aliyewahi kushinda tunzo ya Amani ya Nobel, ajaribu kila awezalo ili kuungwa mkono na Mabudha hao wenye misimamo mikali na baadhi ya mirengo ya kijeshi badala ya kufikiria kuyapatia ufumbuzi matatizo ya Waislamu wa Rohingya. Weledi wa masuala ya kisiasa wanaona kuwa, hatua ya Ofisi ya Rais wa Myanmar ya kuwasilisha taarifa inayowatuhumu Waislamu wa Rohingya kuwa wamefanya uasi na kuasisi mirengo ya kimadhehebu yenye misimamo ya kuchupa mipaka inaonyesha kuendelea harakati iliyoratibiwa dhidi ya Waislamu hao katika ngazi ya juu huko Myanmar. Katika hali ambayo haijafahamika ni akina nani waliohusika na shambulio katika kituo hicho cha ulinzi cha mpakani kati ya Myanmar na Bangladesh wala kundi wanalofungamana nalo, kitendo cha viongozi wa Myanmar cha kuwatuhumu Waislamu wa Rohingya kwa kufanya uasi, si tu kuwa si suluhisho la matatizo bali kinachochea hisia kali za Mabudha dhidi ya Waislamu hao; hatua ambayo itafuatiwa na taathira zisizoweza kuzuilika wala kufidiwa.

3461157

captcha