IQNA

Uhusiano wa nchi za Kiislamu

Mapatano ya kuhuishwa uhusiano wa Saudi Arabia na Iran

9:45 - April 07, 2023
Habari ID: 3476824
TEHRAN (IQNA)- Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia wamekutana Alhamisi katika mji mkuu wa China Beijing na kukubaliana kufunguliwa ofisi za uwakilishi wa nchi mbili na kusisitiza utayari wao wa kuondoa vizuizi vinavyokwamisha kupanuliwa mashirikiano baina ya Tehran na Riyadh.

Wakati wa mazungumzo kati ya Iran na Saudi Arabia yaliyofanyika mjini Beijing, nchi hizo mbili zilikubaliana mnamo Ijumaa, Machi 10, kurejesha uhusiano wa kidiplomasia baada ya miaka saba.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi hizo mbili, ilipangwa kuwa mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na Saudi Arabia, watakutana ili kuandaa mazingira ya utekelezaji wa mabadilishano ya mabalozi na kufungua tena balozi katika nchi mbili pamoja na kukamilsha masuala mengine yanayohitajika kwa ajili ya kurejesha uhusiano

Hatimaye baada ya miaka saba, Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Faisal bin Farhan Al Saud, Waziri wa Mashaur ya Kigeni wa Saudi Arabia, wamekutana na kuzungumza rasmi Alhamisi asubuhi mjini Beijing.

Baada ya mkutano huo, wanadiplomasia hao wakuu wa Iran na Saudia walitia saini taarifa ya pamoja katika hafla iliyohudhuriwa na Qin Gang, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa China.

Mazungumzo ya Alhamisi ya ana kwa ana ya Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudia na Iran yamefanyika mwezi mmoja baada ya makubaliano ya Beijing baina ya mataifa haya mawili.

Mazungumzo mara tatu

Kadhalika katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita mawaziri hao wamezungumza mara tatu kwa njia ya simu. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, yote hayo yanaonyesha kuwa, Iran na Saudia yakiwa madola mawili makubwa na muhimu katika eneo la Asia Magharibi na katika ulimwengu wa Kiislamu yameazimia kwa dhati kuhitimisha mzozo na tofauti zilizokuwa zimejitokeza katika uhusiano wao, na hivyo kustawisha mahusiano baina yao. Katika fremu hiyo, Nasser Kanaani Chafi, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema baada ya mazunguumzo ya leo ya Faisal bin Farhan na Hussein Amir-Abdollahian kwamba, sasa uhusiano rasmi baina ya Riyadh na Tehran umeanza.

Nukta nyingine ni kuwa, ajenda za mazungumzo ya leo baina ya Amir-Abdollahian na Farhan yameonyesha hamu na shauku ya Riyadh na Tehran siyo ya kuhuisha uhusiano wa kisiasa tu, bali kupanua ushirikiano baina yao pia katika nyuga za kiutamaduni na kiuchumi na vilevile kuwa na ushirikiano wenye wigo mpana kuhusiana na masuala ya kieneo.

Usalama wa kudumu

Baada ya mazungumzo hayo, Abdollahian ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwamba: Kuanza rasmi uhusiano wa kidiplomasia wa Tehran-Riyadh, kuanzia ushirikiano katika suala la Hija, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, kufunguliwa balozi na ofisi ndogo za kibalozi na kusisitiza juu ya uthabiti, usalama wa kudumu na ustawi wa eneo (Asia Magharibi) ni mambo yaliyoafikiwa na ambayo yapo katika ajenda za pamoja."

Nukta nyingine muhimu ni hii kwamba, katika mazungumzo ya leo ya Amir-Abdollahian na Faisal na kuhuishwa uhusiano wa Saudi Arabia na Iran chimbuko lake ni kuweko udiriki na ufahamu wa pamoja wa viongozi wa nchi mbili kuhusiana na maslahi ya pande mbili na vilevile usalama wa eneo la Asia Magharibi.

Ukweli wa mambo ni kuwa, Tehran na Riyadh zimefikia udiriki na natija moja kwamba, maslahi ya pande mbili hayawezi kudhaminiwa kwa kukuza uadui na kutokuweko uhusiano baina yao, bali hilo litapatikana na kufikiwa katika fremu ya kukuza na kuongeza zaidi kiwango cha ushrikiano.

Mataifa ya Kiislamu

Nukta ya mwisho ni kuwa, matukio ya kisasa katika eneo la Asia Magharibi baada ya makubaliano ya mwezi mmoja uliopita ya Saudia na Iran yamethibitsha kuwa, kadiri mataifa ya Kiislamu yatakapopunguza hitilafu na mizozo katika uhusiano wao na kupiga hatua upande wa ushirikiano na kupanua ushirikiano, basi ndivyo pia uthabti na usalama unapotawala zaidi katika eneo.

Inatarajiwa kuwa, mazungumzo ya leo ya mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia yatakuwa na matokeo mazuri na chanya zaidi kwa usalama na uthabiti wa eneo hili la Asa Magharibi (Mashariki ya Kati).

4131863

captcha