IQNA

Ulimwengu wa Kiislamu

Mapatano baina ya Iran na Saudia yaendelea kuungwa mkono kimataifa

17:53 - March 11, 2023
Habari ID: 3476692
TEHRAN (IQNA)- Makundi mbalimbali ya kieneo yamekaribisha makubaliano ya kurejesha tena uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ufalme wa Saudi Arabia.

Katika mazungumzo yaliyofanyika jana Ijumaa kati ya Iran na Saudi Arabia mjini Beijing, nchi hizo mbili zilikubaliana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia baada ya kukatwa kwa miaka 7.

Kwa mujibu wa makubaliano ya nchi hizo mbili, mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Saudi Arabia watakutana hivi karibuni, na katika kipindi cha ndani ya miezi miwili, watatayarisha mazingira ya kubadilishana mabalozi na kufunguliwa ofisi za kibalozi na mambo mengine yanayohitajika kwa ajili ya kurejesha mahusiano.

Kwa mnasaba huo Mamlaka ya Ndani ya Palestina imekaribisha makubaliano kati ya Saudi Arabia na Iran na kueleza matumaini kuwa makubaliano hayo yatasaidia kuimarisha amani na kujenga mazingira chanya katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Harakati ya Jihad Islami ya Palestina pia imesema: Tunatumai kuwa makubaliano haya yataunga mkono haki ya watu wa Palestina ya kupambana kwa ajili ya kurejesha haki zao za kihistoriana na kuwa na matokeo chanya kwa kadhia ya Palestina.

Ikikaribisha makubaliano kati ya Iran na Saudi Arabia, Harakati ya Ubunifu wa Kitaifa ya Palestina imezitaka nchi za eneo la Magharibi mwa Asia kufanya juhudi za pamoja za kuunga mkono mapambano ya ukombozi ya Palestina.

Awali, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, HAMAS, ilikuwa imetoa taarifa ikipongeza makubaliano ya kurejesha uhusiano kati ya Tehran na Riyadh.

Tarehe 3 Januari 2016, Saudi Arabia ilikata uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran kwa kisingizio kwamba baadhi ya watu walishambulia ubalozi na ofisi ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Tehran na Mashhad.

4127247

Kishikizo: iran saudi arabia hamas
captcha