IQNA

Sera za Kigeni Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran asema atakutana na mwenzake wa Saudi hivi karibuni

21:41 - March 19, 2023
Habari ID: 3476727
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametangaza kuwa, atakutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia mnamo siku chache zijazo na akasema: "tulikubaliana kuwa jumbe za kiufundi za pande zote mbili zitembelee balozi na balozi ndogo na kufanya maandalizi ya kivitendo ya kufunguliwa tena balozi hizo."
Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari alipozungumzia mafanikio makubwa zaidi ya sera za nje ya serikali katika mwaka 1401 Shamsia, na kubainisha kwamba "katika uwanja wa diplomasia ya uchumi, tunashuhudia ongezeko kubwa la kiwango cha mabadilishano ya kibiashara, kiasi kwamba katika nchi mbili tu jirani, kwa upande wa moja kati ya hizo, kiwango cha mabadilishano ya kibiashara kimefika dola bilioni 14, na katika nchi nyingine ni dola bilioni 22.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, katika uhusiano wa kisiasa na majirani, katikati ya mwaka 1401, uhusiano wa nchi mbili jirani za Imarati na Kuwait na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulipandishwa hadi ngazi ya balozi; na katika siku zilizopita, tulishuhudia Iran na Saudi Arabia zikirejea kwenye uhusiano wa kawaida".

Kuhusu matarajio ya kufikiwa makubaliano ya nyuklia, Amir-Abdollahian amesema, "jukumu la asili la vyombo vya kidiplomasia ni kufanya jitihada kwa ajili ya kuondolewa vikwazo, na kuna mpango mezani ambao ninatumai katika wiki zijazo tutaweza kuwaletea habari rasmi wananchi wa Iran na tutatumia kila fursa ili kupata mafanikio kwa ajili ya taifa kwa kiwango cha juu kabisa".

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, katika safari yake ya Manama mji mkuu wa Bahrain, Sultan wa Oman alipendekeza mpango na wazo la kurejeshwa katika hali ya kawaida uhusiano kati ya nchi mbili za Iran na Bahrain. Takriban miezi miwili iliyopita, makubaliano ya awali yalifikiwa kupitia njia hii, kwa jumbe za kiufundi za Iran na Bahrain kutembelea balozi za nchi mbili".
Amir Abdollahian amesisitiza kwa kusema, "tunakaribisha kurejea uhusiano wa kawaida na nchi jirani na nchi za eneo hili, na ninatumai kuwa baadhi ya vizuizi vilivyopo katika njia ya uhusiano wa Tehran na Manama vitaondolewa na kuweza kupigwa hatua mwafaka katika njia hii pia.
4129086
captcha